Makala

MALENGA WA WIKI: Lemmy Karisa aliusia wanawake wakipenda wasisite kusema

June 28th, 2020 2 min read

Na HASSAN MUCHAI

LEMMY Chengo Karisa anayetumia lakabu yake “Siko Mbali’’ ni mshairi mkongwe kutoka Kaunti ya Kilifi ambaye atakumbukwa daima kutokana na mashairi yake ya maliwazo yaliyojaa ujumbe na uchungu tele.

Chengo ambaye nyakati za miaka ya ‘80 alianza utunzi akiwa kijana mdogo, sasa ni mtu mzima anayetegemewa na jamii yake kwao Kilifi.

Ingawa hajitokezi sana kwenye vyombo vya habari, Karisa ni mtetezi sugu wa lugha ya Kiswahili anayechukizwa na baadhi ya mashairi na washairi “wa kisasa’’.

Anasema nyakati zao, watunzi walipenda kushauriana ili kuiboresha fani hii.

Hata hivyo, anasikitishwa zaidi na kufariki kwa washairi wengi aliotunga nao nyakati zake. Kufa kwao Abdallah Chombo, Kizere, Musa Mzenga, A Shamte, Mwalim Mbega, Rudisi Musyimi, Hajji Dhadho, Sheikh Agola na wengine ni pigo kubwa kwa jukwaa la washairi.

Analia na kuona uchungu kumkosa mshairi mwenzake Mike Mturi Ngolya kutoka Kambe Ribe, Kilifi.

“Naomba mtu aliye na habari kumhusu Mturi Ngolya kutujuza alikoenda ili tuondoe mashaka tuliyo nayo sasa,” anasema Karisa.

Hata hivyo, “Siko Mbali’’ anafurahia kuwaona watunzi wa nyakati hizo kutoka Kilifi ambao bado wanaendelea kutunga.

Anamsifu sana Kazungu Baya Samuel, Rajab Pilau, Mohammed Khamis na wengineo kwani bado wanaipeperusha bendera ya Kilifi hewani.

Ijapokuwa Karisa ametunga mashauri mengi sana, shairi lake alilotunga miaka ya ‘80 ‘Unga wa kilo kupima’ lingali kwenye hisia zake.

Shairi hilo lililochapishwa katika Taifa Leo lilifanya apate uungwaji mkono na washairi wenzake nyakati hizo.

Shairi hilo lilikuwa likielezea madhila waliyokuwa wakipitia Wakenya kutokana na kupanda kwa bei ya vitu madukani na hata sokoni. Itakumbukwa kwamba huu ndio wakati serikali ilipoweka huru bei ya bidhaa na wafanyabiashara wengi laghai wakachukua nafasi hiyo kuwaibia Wakenya.

Isitoshe, Mzee Chengo Karisa alirejea na shairi lingine mwaka 1991 kuwasuta baadhi ya walimu kutokana na tabia ya kuwaadhibu sana watoto. Alifoka kuwa walimu hutumia nguvu sana kuadhibu wanafunzi na kuaga dunia kutokana na vichapo kama hivyo.

 

Waalimu mwachukiza, mnapo rudi watoto,

Hamuachi kuwaliza, kwa kuwacharaza ngoto,

Ngui mnawaumiza, na hamtumii ufito,

Baadhi ya waalimu, adhabu mmezidisha.

Mtoto anapokosa, sawa ni achapwe fito,

Si mkono kumgusa, makofi ngumi na ngoto,

Ni adhabu gani sasa, mbona hamfati wito,

Baadhi ya waalimu, adhabu mmezidisha.

Akiwa ni wako mwana, utasikia tototo?

Kweli ni vibaya sana, mwisho wake ni majuto,

Inaleta kukosana, machunguye ni mazito,

Baadhi ya waalimu, adhabu mmezidisha.

Utamkuta mwalimu, ana mpiga mtoto,

Na kosa si la mhimu, amsugua magoto,

Amri haja salimu, ampiga ngumi nzito,

Baadhi yenu walimu, adhabu mmezidisha.

 

Kuna wakati Chengo Karisa alipotunga shairi ‘Wanawake mkipenda’ lililomtia matatani.

Alitaka kuwaambia wanawake wajitokeze wazi wazi wanapopenda kitu wala si kuwa na kisebu sebu.

Kwamba, endapo mwanamke amependa mtu hana budi kumwambia mtu huyo ili ajue.

Shairi hili lilimpa ghera zaidi na akatunga mengine yaliyobahatika kuchapishwa katika Taifa Leo.

Tofauti na washairi wa siku hizi wanaopenda kutumia sana mkondo wa tarbia, Mzee Karisa amewahi kujaribu kusafiria bahari za takhmisa, tenzi, tathlitha, hamziya na kadhalika.

Ni mwepesi wa kuyajadili maswala yanayokabili maisha ya kila siku ya mwanadamu.