Malengo yangu ni kushindia PSG taji la kwanza la UEFA – Messi

Malengo yangu ni kushindia PSG taji la kwanza la UEFA – Messi

Na MASHIRIKA

LIONEL Messi amesema kubwa zaidi katika maazimio yake kwa sasa ni kuongoza miamba wa soka ya Ufaransa, Paris Saint-Germain (PSG) kutwaa ufalme wa Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) kwa mara ya kwanza.

Raia huyo wa Argentina mwenye umri wa miaka 34 alishinda mataji manne ya UEFA akivalia jezi za Barcelona, mara ya mwisho ikiwa 2015.

PSG wangali wanasaka taji lao la kwanza la UEFA baada ya kuzidiwa maarifa na Bayern Munich kwenye fainali ya 2020 jijini Lisbon, Ureno. Walibanduliwa na Manchester City kwenye nusu-fainali za kipute hicho mnamo 2020-21.

“Malengo na ndoto yangu ni kushinda taji la UEFA kwa mara nyingine,” akasema mfumaji huyo. Akiwa miongoni mwa wanasoka bora zaidi duniani kwa sasa, Messi alifunga mabao 672 kutokana na mechi 778 ndani ya jezi za Barcelona.

Messi anajivunia kutwaa taji la Ballon d’Or mara sita na kujizolea mataji 35 wakati wa kuhudumu kwake uwanjani Nou Camp.

Baada ya ukiritimba wao katika Ligue 1 kukomeshwa na Lille mnamo 2020-21, PSG wamejinasia huduma za wanasoka Sergio Ramos, Georginio Wijnaldum, Messi, Achraf Hakimi na Gianluigi Donnarumma.

Kuwapo kwa Messi, Neymar Jr, Kylian Mbappe, Mauro Icardi na Angel di Maria kambini mwa PSG kunafanya klabu hiyo kuwa kikosi kinachojivunia mafowadi matata zaidi duniani.

Rais wa PSG, Nasser Al-Khelaifi anaamini kwamba kutua kwa Messi uwanjani Parc des Princes kunampa Mbappe kila sababu ya kusalia kambini mwa waajiri wake wa sasa kwa muda mrefu japo anawaniwa pakubwa na Real Madrid.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Sababu za Ruto kutia miamba 5 tumbojoto

IEBC motoni kuhusu pesa za kampeni