MALEZI KIDIJITALI: Muda kwa mitandao usipite saa 1 kwa siku

MALEZI KIDIJITALI: Muda kwa mitandao usipite saa 1 kwa siku

Na PAULINE ONGAJI

WAZAZI wengi wamekuwa wakiachilia watoto wao kutazama runinga, kudurusu mtandao, kucheza michezo ya video au kutumia laptopu kwa saa nyingi bila kujua wanawaweka kwenye hatari.

Wataalamu wa malezi dijitali wanasema kwamba japo ni vigumu kuepuka matumizi ya vifaa vya kidijitali enzi hizi za maendeleo ya tekinolojia, watoto hawafai kuruhusiwa kuzama kwa mtandao au kompyuta kwa saa nyingi.

“ Wazazi wanafaa kuhakikisha watoto wa umri wa miaka miwili hadi mitano hawatumii muda wa zaidi ya saa moja kwa siku katika mtandao au runinga. Kwa hakika, wanafaa kutumia chini ya saa moja kwa kifaa chochote cha dijitali na wawe chini ya uangalizi wa mzazi,” aeleza mtaalamu wa malezi dijitali, Susana Ross.

Wataalamu wanasema sababu ya wazazi kutakiwa kuwa ngangari watoto wao wakizama kwenye vifaabebe ni kutafsiri na kujadili wanachofanya.

“Kumuacha mtoto kushughulika na vifaa vya dijitali peke yake kwa saa nyingi ni sawa na kutelekeza jukumu la ulezi,” asema Ross.

Anasema kuwa kwa watoto wa umri wa miaka sita na zaidi, wazazi wanahitaji kuwawekea mpango wa kutumia vifaa vya kidijitali kuhakikisha hawakosi muda wa kutosha wa kulala na kucheza na hata kujadiliana mambo baina yao, wazazi na marafiki.

“Wataalamu wa malezi dijitali wako na wasiwasi kwamba muda ambao watoto wanatumia wakizama katika vifaa vya kidijitali unachukua wa kujijenga kijamii, kufikiria na michezo ya kuimarisha afya ya mili na akili zao,” aeleza Ross.

Anasema kuwa watoto wanaotumia muda mwingi katika mtandao au wakitazama runinga huwa na mili minene jambo ambalo ni hatari kwa afya yao.

“Hivyo basi, wazazi hawana budi kuthibiti muda ambao watoto wao wanatumia kwenye mtandao ili wapate muda wa kushiriki michezo kwa manufaa ya afya zao,” aeleza.

Anasema jukumu la wazazi kwa ulezi enzi hizi haliwezi kuepukika.

You can share this post!

HUKU USWAHILINI: Hata sisi tumepigwa na hii corona,...

JUKWAA WAZI: Suala la aliye mkarimu kati ya Raila na Ruto...

T L