Habari

Mali inayokadiriwa kuwa ya thamani ya Sh12 milioni yaharibiwa na moto shuleni Koyonzo

November 16th, 2019 1 min read

Na SHABAN MAKOKHA

MALI inayokadiriwa kuwa ya thamani ya Sh12 milioni imeharibiwa baada ya moto wa usiku wa manane katika Shule ya Sekondari ya Wavulana ya Koyonzo, kaunti ndogo ya Matungu, Kaunti ya Kakamega.

Mwenyekiti wa Bodi ya Usimamizi wa shule hiyo Bw Francis Namuswa amesema moto huo wa saa saba usiku wa kuamkia Jumamosi saa umeteketeza chumba ambamo kulikuwa kumewekwa mali ya wanafunzi wa kidato cha kwanza, pili na cha tatu walio katika likizo ya muhula wa tatu.

“Kando na vifaa na mali ya wanafunzi, jenereta ya shule na nafaka ni miongoni mwa mali iliyoharibika,” amesema Bw Namuswa.

Ingawa hivyo, amesema watahiniwa wote 250 shuleni humo wa mtihani wa kitaifa wa kidato cha nne (KCSE 2019) wangali salama na dhamira yao ni kuendelea kufanya mtihani kwa utulivu.

OCPD wa Matungu Bw Alex Ndili amethibitisha kwamba malazi ya wanafunzi na vifaa vya kutumika darasani ni miongoni mwa mali iliyoharibiwa na moto huo.

Amesema wanafunzi saba wanahojiwa na polisi katika juhudi za kuelewa kiini cha moto huo.

“Hawajakamatwa lakini wanasaidia polisi na uchunguzi kisha baada ya hapo wataruhusiwa kujiandaa kwa mtihani wao,” amesema Bw Ndili.

Mkasa huu wa moto unajiri siku chache baada ya kutibuliwa hali ya mshikemshike watahiniwa walipolalamika kuhusu kuangaziwa sana na wasimamizi wa mtihani huo wa kitaifa.