Habari Mseto

Mali ya mamilioni yateketea Gikomba tena

June 25th, 2020 1 min read

Na PETER CHANGTOEK

WAFANYIBIASHARA katika soko la Gikomba, kwa mara nyingine tena, wanakadiria hasara baada ya mali zao kuteketea Alhamisi kufuatia kuzuka kwa moto uliowasababishia hasara kubwa.

Mali ya mamilioni ya pesa iliteketea kwa moto huo, ambao chanzo chake hakikubainika bayana mara moja.

Baadhi ya wafanyabiashara hao walisema kuwa moto huo ulisababishwa na stima, huku wengine wakidai kwamba huenda ulisababishwa na watu waliouwasha kimakusudi.

Wafanyibiashara hao, ambao wengi huishi katika mitaa kama vile; Huruma, Kariobangi, Mlango Kubwa, Mathare, Dandora, Umoja, Kayole; miongoni mwa mitaa mingineyo, walishurutika kusafiri usiku wa manane kwa kutumia pikipiki kutoka maskani yao, ili kufika katika eneo hilo la biashara, ili kujaribu kuziokoa mali zao, lakini wengi wao hawakufanikiwa kuziokoa.

Miongoni mwa mali zilizoteketea kwa moto huo ni nguo za mitumba, nafaka kama vile maharagwe, dengu, mbaazi na mali nyinginezo.

Mazimamoto kutoka Kenya Police, Kaunti ya Nairobi, National Youth Service (NYS), ni kati ya yale yaliyokuwa yakitoa huduma zao za kuuzima moto huo, uliokuwa ukienea kwa kasi mno.

Aidha, helikopta ya jeshi lilisaidia kuuzima moto huo kutoka angani, ambapo ulidhibitiwa saa tano za mchana.

Kwa mujibu wa baadhi ya wafanyibiashara pamoja na wale walioshuhudia tukio hilo ni kuwa, moto huo ulizuka mwendo wa saa nane za usiku wa kuamkia Alhamisi.

Si mara ya kwanza kwa soko hilo kuchomeka na mali za thamani kubwa kuteketea na kuwasababishia wafanyibiashara hasara kubwa mno.

Dkt Karanja Kibicho pamoja na maafisa wengine wa serikali waliwasili katika soko hilo ili kutathmini yaliyojiri.