Mali ya Sirma hatarini kuuzwa na madalali

Mali ya Sirma hatarini kuuzwa na madalali

Na JOSEPH OPENDA

ALIYEKUWA waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Musa Sirma huenda akapoteza mali ya thamani ya mamilioni kwa wapiga mnada, baada ya kushindwa kulipa gharama ya kesi ya uchaguzi.

Kampuni ya mnada ya Saddabri Auctioneers tayari imetoa ilani ya kuendelea na shughuli hiyo, ili kukusanya Sh754,000 kwa niaba ya Mbunge wa Eldama Ravine, Bw Moses Lessonet.

Hii ni baada ya kukamilika kwa notisi ya siku 10 ya kulipa deni hilo iliyotolewa na korti mnamo Oktoba 6 mwaka huu.“Tunakuamrisha uambatanishe mali yenye thamani sawa na pesa unayodaiwa na Bw Lessonet,” ikasoma sehemu ya amri ya korti.

Kampuni hiyo ya mnada ikishirikiana na ile ya mawakili ya Gordon Ogolla na Kikoech tayari imetaja ng’ombe wa maziwa 20 wanaogharimu Sh35,000 kila mmoja, gari moja aina ya Toyota Prado na magari mengine mawili ili kukusanya Sh754,000 anazodaiwa na Bw Lessonet.

Bw Sirma ambaye alimenyana na Bw Lessonet kutaka ubunge wa Eldama Ravine, Baringo kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2017, alipoteza kesi hiyo kutokana na ukosefu wa ushahidi.Mnamo 2018, Mahakama ya mjini Kabarnet ilimwamuru kulipa Sh6 milioni, kwa Bw Lessonet, Tume ya Uchaguzi na Mipaka nchini (IEBC) na Afisa Msimamizi wa Uchaguzi Peter Kuria.

Mbunge huyo wa zamani alipinga uamuzi huo na kuenda katika mahakama Kuu ya Kabarnet. Katika rufaa yake, Bw Sirma alinuia kusimamisha amri ya korti iliyotolewa Machi 4, 2018 kuhusiana na kesi hiyo.

Alidai kuwa mahakama ilitumia mbinu ya kuchelewesha kesi, kama njia ya kutoa nafasi kuvuruga uamuzi. Aliamini kwamba kulikuwa na mkono wa maafisa wakuu serikalini kuhusiana na hatima ya kesi yake.

“Sikubaliani na uamuzi huu. Ninajua kwamba matokeo ya rufaa hii yangebadilisha kabisa hali ya kisiasa nchini siku zijazo,” akasema wakati huo.Jaji wa Mahakama Kuu ya Kabarnet, Justus Bwonwong’a alitupilia mbali ombi lake na kumwamuru alipe deni hilo, jinsi korti ilivyoamua hapo awali.

Kutokana na uamuzi huo, Bw Lessonet kupitia kwa wakili wake Kipkoech Ng’etich alipata huduma za madalali baada ya Bw Sirma kukosa kulipa pesa hizo.Bw Sirma hata hivyo, alirejea mahakamani mwaka wa 2019 akitaka kupinga tangazo la madalali ambao aliwashutumu kwa kutangaza thamani ya mali yake.

Alidai kuwa kwa mfano, gari lake aina ya Prado Land Cruiser, thamani yake ni ya juu kuliko iliyosemekana kwenye ripoti.Hata hivyo, ombi hilo lilitupiliwa mbali na kuruhusu mnada kuendelea.

You can share this post!

CHAKISTA mwenge thabiti wa Kiswahili katika Shule ya Upili...

LEONARD ONYANGO: Ruto, Raila watumie mitandao ya kijamii...

T L