Michezo

Mali yaponea pembamba faini na adhabu kali ya Fifa

June 18th, 2019 1 min read

Na MASHIRIKA

BAMAKO, Mali

TIMU ya taifa ya Mali inaelekea kukwepa marufuku kutoka kwa Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) baada ya Shirikisho la Soka nchini Mali (FEMAFOOT) kuandaa mkutano kumaliza migogoro ndani yake.

Ripoti kutoka nchini Mali zinasema kwamba Mali ilikuwa katika hatari ya kupigwa marufuku na FIFA kutokana na kutofuata maagizo ya FIFA kuhusu usuluhishaji wa mivutano ya uongozi.

Baada ya mazungumzo ya saa 13 mnamo Juni 15, ilikubaliwa kura zifanywe ndani ya siku 60 kuchagua maafisa wapya.

Inasemekana FIFA iliridhishwa na mikakati hii na sasa Eagles, ambayo ndiyo timu ya taifa ya Mali, itashiriki Kombe la Afrika (AFCON) litakalofanyika nchini Misri kutoka Juni 21 hadi Julai 19, 2019.

Mali iko katika Kundi E pamoja na mabingwa wa mwaka 2004 Tunisia, ambao ni mojawapo ya timu zinazopigiwa upatu kutwaa taji, Angola na washiriki wapya kabisa katika AFCON, Mauritania.

Misri yapigiwa upatu mkubwa

Kwingineko, kocha mkuu wa Misri Javier Aguirre amesema yuko tayari kuhama timu hiyo asipoiongoza kutwaa ubingwa katika makala ya 32 ya AFCON mbele ya mashabiki wake.

Mafirauni hao wako katika orodha ya timu zinazopigiwa upatu mkubwa kushinda mashindano haya ya mataifa 24.

Mabingwa hawa mara saba wamemtwikwa majukumu ya kuongoza Misri kutamba nyumbani.

“Wakati huu kile kilicho akilini mwangu ni mechi ya ufunguzi ya AFCON dhidi ya Zimbabwe. Niko na kandarasi na Misri, lakini sioni haja ya kuendelea kunoa Misri isiposhinda Kombe la Afrika,” alisema raia huyo wa Mexico, ambaye aliwahi kushikilia wadhifa wa kocha mkuu wa timu za taifa za Mexico na pia Japan.