Habari Mseto

Malipo yaja, serikali yajaribu kutuliza wakulima wa miwa

January 7th, 2019 2 min read

Na SHABAN MAKOKHA

WAKULIMA wa miwa ambao waliwasilisha miwa yao kwa viwanda vya sukari vinavyomilikiwa na serikali watalipwa fedha zao kati ya Januari na Februari, Gavana wa Kakamega Wycliffe Oparanya amesema.

Gavana huyo, ambaye ndiye naibu mwenyekiti wa jopokazi maalum ambalo lilibuniwa kulainisha sekta hiyo, alisema kuwa ucheleweshaji huo ulisababishwa na Hazina ya Kitaifa.

Alisema kuwa hali hiyo imezua malumbano na uhasama miongoni mwa wadau mbalimbali katika sekta hiyo.

“Tulikuwa tumepanga kuwalipa wakulima Desemba iliyopita, ila kumekuwa na ucheleweshaji uliosababishwa na Hazina ya Kitaifa. Nadhani kwamba tutawalipa wakulima hao mwezi huu, ikiwa si mapema mwezi ujao,” akasema.

Alisema kuwa jopokazi hilo lingali linaendelea kufanya vikao vya kupokea maoni kutoka kwa wadau mbalimbali ili kulainisha sekta hiyo.

Alieleza kuwa kikao kijacho kati ya wanachama wa jopokazi na wakulima kitafanyika mjini Mumias mnamo Januari 15, ambapo amewaalika wadau wote kujitokeza kutoa maoni yao kuhusu mikakati ya kuilainisha sekta hiyo.

Kauli ya Bw Oparanya inajiri huku wakulima wakiendelea kulalama kuhusu kucheleweshwa kutolewa kwa Sh2.6 bilioni kuwalipa kama walivyoahidiwa na Rais Uhuru Kenyatta. Wakulima hao wanadai kwamba wamekosa kuwapeleka watoto wao shuleni kwani hawajalipwa fedha hizo.

Baadhi ya viongozi kutoka eneo la Magharibi wamelikosoa jopokazi hilo kwa kutotimiza malengo yake kwa kipindi cha mwezi mmoja, kama ilivyotangazwa na Rais Kenyatta mnamo Oktoba 20, 2018 lilipozinduliwa. Miongoni mwa viongozi hao ni kiongozi wa ANC Musalia Mudavadi, aliyekuwa Seneta wa Kakamega Boni Khalwale na Waziri wa Michezo Rashid Echesa.

Lakini akizungumza katika Kaunti Ndogo ya Lugari mnamo Jumamosi, Bw Oparanya aliwaomba wakulima kuwa wenye subira, jopokazi hilo linapojaribu kukabili changamoto ambazo zimekuwa zikiikabili sekta hiyo.

“Baadhi ya watu wanadai kwamba fedha za kuwalipa wakulima wa Mumias zilitolewa na Serikali Kuu na zipo katika Serikali ya Kaunti ya Kakamega.

Hata hivyo, ningependa kuwafahamisha kwamba siko katika jopokazi hilo kuangazia masuala ya Kampuni ya Sukari ya Mumias pekee ila kote nchini,” akasema.