Michezo

Malkia Strikers wajifariji kwa kupiga Cameroon

September 30th, 2019 2 min read

Na JOHN KIMWERE

HATIMAYE timu ya Kenya ya Malkia Strikers ilibahatika kuvuna ushindi wa kujifariji kwenye voliboli ya Kombe la Dunia (FIVB) ilipochabanga Cameroon seti 3-1 uwanjani Edion mjini Osaka, nchini Japan mnamo Jumapili.

Vipusa wa kocha, Paul Bitok walipata ufanisi wa alama 25-16, 26-24, 14-25,25-21 licha ya kupoteza mechi kumi mfululizo tena bila kushinda seti hata moja.

Malkia Strikers walizoa ufanisi huo siku moja baada ya kulimwa seti 3-0(25-16,25-21,25-22) na Urusi na kocha huyo kusifia kikosi hicho kwa kuendelea kuimarika.

Kocha huyo alinukuliwa akisema ”Hatujaweza kudhiti mchezo wetu lakini tumeanza kucheza kama miamba mchezo wa kasi.” Pia alisema hayo ni mafanikio makubwa kwa kikosi hicho maana mtindo walioanzisha umeanza kuzaa matunda baada ya kufikisha alama 21, 22 dhidi ya Urusi.

Kadhalika alidokeza kuwa wachezaji hao wameanza kucheza voliboli ya kisasa na katika miaka miwili au mitatu watakuwa pazuri zaidi kufanya kweli.

Warembo hao walipoteza mechi kwa kulazwa seti 3-0 kila moja na

Marekani, Argentina, Uholanzi, Urusi, Korea, Brazil, Uholanzi, Serbia, Jamhuri ya Dominican na Uchina.

Ushindi huo ulisaidia Malkia Strikers kupanda hatua moja na kutua katika nafasi ya 11 kwa alama tatu, moja mbele ya Cameroon.

Cameroon ilisajili pointi hizo mbili baada ya kujitahidi na kushindwa mechi mbili kwa seti 3-2 kila moja mbele ya Jamhuri ya Dominican na Argentina.

Ilikuwa mara ya sita kwa Kenya kushiriki mashindano ya Kombe la dunia licha ya kutofanya vizuri kwenye makala yaliyopita. Ilimaliza mkiani nafasi ya 12 kwenye makala ya 1991,2007 na 2011. Kisha ilibahatika kuibuka ya 11 na kumi mwaka 1995 na 2015 mtawalia.

Mashindano hayo yaliyokamilika Jumapili, Uchina iliibuka mabingwa kwa kuandikisha alama 32 baada ya kushinda mechi zote 11.

Uchina ulisajili ushindi wa seti 3-0 mara tisa, seti 3-1 na 3-2 mara moja kila moja, nayo Marekani ilimaliza ya pili kwa kuzoa pointi 28, tano mbele ya Urusi mabingwa wa 1973.

Marekani ilijivunia kuzoa ufanisi wa mechi tano kwa seti 3-0, kisha kuvuna seti 3-1 na 3-2 mara tatu na mbili mtawalia.