Michezo

Malkia Strikers walemewa na Cameroon

July 15th, 2019 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

MALKIA Strikers ya Kenya imeridhika na medali ya fedha kwa mara ya pili mfululizo kwenye Kombe la Voliboli ya Afrika ya Wanawake baada ya kutupa uongozi mara mbili katika seti ya tano na kuzimwa kwa seti 3-2 dhidi ya Cameroon katika fainali kali jijini Cairo nchini Misri, Jumapili usiku.

Mechi hii ilikuwa sawa na marudiano baada ya Kenya kupepeta Cameroon 3-2 katika mechi yake ya mwisho ya makundi.

Tatizo kubwa lililochangia Kenya kupoteza ni kupiga mipira mibovu ilipopata nafasi ya kuanzisha na pia ulinzi wake ulikuwa ukivuja, hasa kuzuia makombora ya Cameroon.

Mabingwa wa Afrika mara tisa Kenya walianza fainali vibaya walipolemewa kwa seti ya kwanza 25-17.

Walijikakamua na kusawazisha seti 1-1 waliposhinda seti ya pili 27-25, lakini wakazidiwa maarifa tena katika seti ya tatu 25-23.

Wakenya walisawazisha tena 2-2 baada ya kutwaa seti ya nne 25-23, lakini wakaishiwa ujanja katika setiya mwisho baada ya kupoteza uongozi wa alama 3-1 na 14-13.

Kabla ya kichapo hiki, Kenya ilikuwa imeshinda mechi zake zote za makundi dhidi ya Algeria 3-0, Botswana 3-0 na Cameroon 3-2 na kupepeta Senegal 3-0 katika nusu-fainali. Nayo Cameroon ilikuwa imepoteza dhidi ya Kenya pekee na kulima Botswana na Algeria 3-0 katika mechi za makundi na wenyeji Misri 3-0 katika nusu-fainali.

Kenya inashikilia rekodi ya mataji mengi ya kombe hili baada ya kushinda kutoka mwaka 1991-1997, 2005-2006 na 2011-2015.

Fainali kati ya Kenya na Cameroon ilitanguliwa na Senegal kuzoa medali ya shaba baada ya kulemea mabingwa mara tatu Misri 3-1 (25-17, 25-17, 14-25, 28-26).