Malkia Strikers wang’aria Burundi mtihani mkali dhidi ya Rwanda nusu-fainali ukinukia

Na AGNES MAKHANDIA

KENYA itamenyana na wenyeji Rwanda katika mojawapo ya mechi za nusu-fainali za Kombe la Afrika la voliboli ya kinadada mnamo Septemba 18 baada ya kulipua Burundi ikimaliza ya pili katika Kundi B, Alhamisi.

Dhidi ya Burundi, kocha Paul Bitok aliendelea kuwapa wachezaji wake wote nafasi ukumbini Kigali Arena.

Alianzisha libero Elizabeth Wanyama, mzuiaji wa kati Lorraine Chebet na mshambuliaji wa pembeni kulia Emmaculate Chemtai na kuwaweka kitini Agrippina Kunda, Sharon Chepchumba na Esther Mutinda.

Kenya maarufu kama Malkia Strikers, ambao walilipua Tunisia 3-0 Septemba 15, waliongoza Burundi katika mapumziko yote mawili rasmi kwa alama 8-3 na 16-7.

Bitok kisha alipumzisha Edith Wisa, Leonida Kasaya na Lusenaka na kujaza nafasi zao na Yvonne Sinaida, ambaye alikuwa akishiriki mechi yake ya kwanza kabisa, chipukizi matata Veronica Adhiambo na Mutinda, huku Kenya ikilemea Burundi kwa alama 25-8.

Katika seti ya pili, Adhiambo alivuna alama nyingi kwa makombora makali ya kuanzisha mechi ambayo Burundi ilitatizika kupokea.Kenya kisha iliongoza 8-2 katika mapumziko ya kwanza, huku Pamela Masaisai, Sinaida na Mutinda wakisaidia katika kufungua mwanya wa 14-6 kupitia makombora makali.

Mashambulizi hafifu ya Burundi yalikuwa zawadi kwa Kenya iliyonyakua seti hiyo kwa alama 25-9.Mambo hayakuwa tofauti katika seti ya tatu, ingawa Kenya iliongoza mapumziko ya kwanza pembemba 8-5.

Masaisai na Adhiambo, ambao walifurahisha, kisha walisaidia katika Kenya kuongeza mwanya hadi 14-8.Burundi haikufaulu katika kuzuia mashambulizi ya Kenya ambayo ilifurahia kuingia mapumziko ya pili kifua mbele 16-7 kabla ya kukamilisha kazi katika seti hiyo kwa alama 25-11.

Baada ya mechi, Bitok alisema kuwa anatarajia timu yake kuimarika katika mechi zijazo. “Mpango wangu ulikuwa kupumzisha wachezaji tegemeo dhidi ya Burundi kabla ya kibarua kigumu kutoka kwa waajiri wangu wa zamani Rwanda.

Kuchezesha wachezaji wote ni lengo langu la kuhakikisha wale wapya wanapata motisha. Kwa sababu hiyo, niliwapa nafasi Sinaida, Adhiambo na Chemtai.” Bitok alipumzisha nyota Chepchumba, Moim na Kundu katika mchuano huo wote.

Ushindi dhidi ya Burundi uliwezesha Kenya kumaliza nambari mbili katika kundi lake kwa alama tisa, tatu nyuma ya mabingwa watetezi Cameroon ambao hawajapoteza mchuano. Rwanda wanaongoza Kundi A.