Michezo

Malkia Strikers wapigwa seti 3-0 na Dominican Republic

September 22nd, 2019 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

KENYA ilipoteza mechi yake ya 37 tangu ianze kushiriki Kombe la Dunia mwaka 1991 baada ya Malkia Strikers kuchabangwa na Jamhuri ya Dominican kwa seti 3-0 katika makala ya mwaka 2019 yaliyoingia siku ya tisa nchini Japan, Jumapili.

Malkia Strikers ya kocha Paul Bitok iliingia mechi dhidi ya Dominican ikitumai kufanya vyema baada ya kupoteza kwa seti 3-0 dhidi ya Marekani, Uholanzi, Serbia, Brazil na Argentina.

Hata hivyo, mambo hayakuwa tofauti ilipobwagwa bila kushinda seti kwa alama 25-17, 25-19, 25-19. Leonida Kasaya alifungia Kenya alama nyingi (12) naye Sharon Chepchumba Kiprono akachangia tisa.

Bethania De La Cruz De Pena na Brayelin Elizabeth Martinez walikuwa wafungaji bora wa Dominican. Walifunga alama 18 na 13, mtawalia.

Kichapo hiki kilikuwa cha tatu mfululizo cha Kenya dhidi ya Dominican katika Kombe la Dunia baada ya kupoteza 3-0 mwaka 2007 na kupokea dozi sawa na hiyo katika makala yaliyopita mwaka 2015.

Baada ya kipigo hicho, kocha mkuu wa Kenya, Paul Bitok alikiri kusikitishwa na matokeo. Amenukuliwa na Shirikisho la Voliboli Duniani (FIVB) akisema, “Tunasikitika sana kupoteza mchuano huu. Tulianza kupiga hatua katika mechi iliyopita. Tulitaka kucheza vyema zaidi, lakini tukalimwa 3-0. Tunataka kuimarisha tunavyopokea mipira na kasi yetu ya mchezo. Lengo letu ni kuimarisha mchezo. Lazima tulenge siku za usoni kuwa washindani halisi.”

Nahodha wa Malkia Strikers, Mercy Moim, ambaye pamoja na seta Janet Wanja ni miongoni mwa wachezaji watano wanaoshikilia rekodi ya kuwa Kombe la Dunia kwa muda mrefu (mara nne), alitofautiana kidogo. “Siwezi kusema tulicheza vibaya ama vizuri. Waliposhambulia, tulitatizika kuzuia makombora yao. Hata hivyo, tunatumai kabla ya mashindano haya kufika tamati tutakuwa tumepata matokeo bora.”

Kenya imecheza mechi 40 katika Kombe la Dunia tangu ifuzu kwa mara ya kwanza mwaka 1991. Ilishinda mechi moja mwaka 1995 ilipopiga Misri na kuzoa ushindi mara mbili mwaka 2015 ilipolemea Algeria na Peru.

Malkia Strikers itarejea uwanjani Septemba 23 kumenyana na wenyeji Japan mjini Sapporo.