Malkia Strikers waramba sakafu tena

Malkia Strikers waramba sakafu tena

Na GEOFFREY ANENE

KENYA ilikubali kichapo cha saba mfululizo kwenye Kombe la Dunia la voliboli ya wanawake baada ya kulimwa na wenyeji Japan kwa seti 3-0 Jumatatu mjini Sapporo.

Malkia Strikers, ambayo itavaana na China leo Jumanne, iliingia mchuano dhidi ya Japan ikiuguza vichapo vya dozi sawa na hiyo dhidi ya Marekani, Uholanzi, Serbia, Brazil, Argentina na Jamhuri ya Dominican.

Hata hivyo, warembo wa kocha Paul Bitok walionyesha kuimarika zaidi dhidi ya Japan kwa mara ya kwanza wakifikisha alama 20 katika seti mbili. Waliandikisha alama 25-18, 25-22, 25-20 katika seti hizo.

Kabla ya hapo, Kenya ilikuwa imefikisha alama 20 ilipolimwa na Marekani (25-14, 25-20, 25-14) na Brazil (25-20, 25-17, 25-14). Haikufikisha alama 20 dhidi ya wapinzani wengine. Kilichosaidia Kenya zaidi kuimarika ni uzuiaji wa mipira kwenye neti na pia kupunguza makosa.

Bitok aliwaanzisha Jane Wacu, Leonida Kasaya, Sharon Chepchumba, Trizah Atuka, nahodha Mercy Moim, Edith Wisa na Agrippina Kundu katika mechi hii ambayo Wisa aliibuka mfungaji bora wa Kenya kwa alama 13, sawa na Mjapani Sarina Koga.

Kukamilisha kampeni

Malkia Strikers, ambayo mwezi uliopita ilinyakua taji la michezo ya Afrika (African Games) nchini Morocco, bado inatafuta pointi yake ya kwanza.

Kwa sasa, Kenya iko mkiani bila alama.

Itakutana na Korea Kusini mnamo Septemba 27 na kukamilisha kampeni dhidi ya mabingwa wa Afrika Cameroon mnamo Septemba 29.

Kwa jumla, Kenya imekuwa na rekodi mbaya kwenye kombe hili linalofanyika kila baada ya miaka minne.

Ilianza kushiriki mashindano haya mwaka 1991. Ilipoteza mechi zote mwaka huo kabla ya kulemea Misri katika makala yaliyofuata mwaka 1995.

Ilirejea katika kombe hili mwaka 2007 na kukaribishwa kwa vichapo 11 mfululizo kabla ya kupotea tena na kisha kujitokeza mwaka 2015 iliposhinda Peru na Algeria na kupoteza mechi tisa.

Matumaini ya Kenya kuzoa ushindi katika makala ya mwaka huu yanazidi kudidia siku zinazoendelea na itahitajika kufanya kazi ya ziada katika mechi zilizosalia.

  • Tags

You can share this post!

KK Homeboyz yapiku Gor, Bandari katika ngazi ya ligi

TEKNOLOJIA: Wanafunzi wako tayari, nani atawafundisha...

adminleo