Michezo

Malkia Strikers watakaosaka ubingwa Japan watajwa

August 15th, 2018 2 min read

Na GEOFFREY ANENE

KOCHA Japheth Munala ametangaza kikosi cha Malkia Strikers kitakachoshindania taji ubingwa wa mashindano ya voliboli ya dunia ya wanawake yakatakayofanyika nchini Japan mnamo Septemba 29 hadi Oktoba 20, 2018.

Nyota Jane Wacu na Jannet Wanja watabadilishana majukumu ya useta baada ya kupata tiketi mbili za idara hiyo. Washambuliaji matata Mercy Moim na Noel Murambi wamo kikosini kama kawaida sawa na wazuiaji tegemeo Edith Wisah na Trizah Atuka.

Munala amezindua kikosi hicho chake cha mwisho katika ukumbi wa kimataifa wa Kasarani jijini Nairobi, Jumatatu. Timu ya Kenya inapanga kuelekea nchini Japan mapema kupiga kambi ya mazoezi nchini humo.

Wakati huo huo, habari kutoka jijini San Juan zinasema Puerto Rico imepata kocha mpya kwa jina Jose Mieles. Kocha huyu aliwahi kuongoza timu hii kati ya mwaka 2013 na 2015. Alipewa majukumu yakuiongoza tena hapo Agosti 13, 2018.

Puerto Rico iko katika kundi D pamoja na Brazil, Serbia, Jamhuri ya Dominican, Kazakhstan na Kenya, ambayo mara ya mwisho ilishiriki mashindano haya ya dunia ni mwaka 2010 nchini Japan.

Mwaka huo, Kenya ilivuta mkia katika kundi lake baada ya kupoteza mechi tano mfululizo ikiwa ni pamoja na kupepetwa kwa seti 3-0 dhidi ya Brazil na pia Puerto Rico. Malkia iliorodheshwa ya mwisho katika mashindano haya ya mataifa 24.

Makala ya mwaka 2018 yatafanyika kati ya Septemba 29 na Oktoba 20 nchini Japan. Kenya na Cameroon zilifuzu kuwakilisha Bara Afrika.

Warembo wa Munala walilemewa kwa seti 3-0 na Cameroon katika fainali jijini Yaounde mwezi Oktoba mwaka 2017, ingawa timu zote mbili zilikuwa zimeshafuzu kwa kushinda mechi zao za nusu-fainali. Mechi za Kundi D zitaandaliwa mjini Hamamatsu.

Cameroon, ambayo ilipeperusha bendera ya Afrika katika makala ya mwaka 2014 kwa pamoja na Algeria, iko katika Kundi A pamoja na Argentina, Ujerumani, Japan, Mexico na Uholanzi.

Kikosi cha Malkia Strikers:

Maseta – Jane Wacu na Jannet Wanja;

Wazuiaji wa katikati – Edith Wisah, Trizah Atuka, Lorine Chebet na Christine Siwa;

Washambuliaji wa pembeni kushoto – Mercy Moim, Noel Murambi, Sharon Chepchumba na Leonida Kasaya;

Washambuliaji wa pembeni kulia – Violet Makuto na Emmaculate Chemtai;

Malibero – Elizabeth Wanyama na Agripina Kundu.