Michezo

Malkia Strikers yalenga kulipiza kisasi dhidi ya Cameroon

July 11th, 2019 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

MALKIA Strikers ya Kenya italenga kulipiza kisasi dhidi ya mabingwa watetezi Cameroon katika mechi ya mwisho ya Kundi B ya mashindano ya voliboli ya wanawake ya Bara Afrika Alhamisi usiku jijini Cairo nchini Misri.

Warembo wa Shaileen Ramdoo, ambao walipepetwa kwa seti 3-0 katika fainali ya makala yaliyopita ya mwaka 2015, wataingia mchuano huu na motisha ya juu baada ya kuzamisha washindi wa mwaka 2009 Algeria 3-0 (25-19, 25-21, 25-21) Julai 9 na Botswana 3-0 (25-16, 25-18, 25-11) Julai 10 katika mechi zao mbili za kwanza kwenye kundi hili.

Hata hivyo, Wakenya wako nyuma ya Cameroon kwa tofauti ya alama walizoandikisha katika seti zao dhidi ya Botswana na Algeria waliobwagwa 3-0 (25-12, 25-17, 25-10) na 3-0 (25-21, 25-5, 26-24), mtawalia.

Malkia Strikers kwenye maombi kabla ya mchuano wa awali. Picha/ Hisani

Cameroon imeapa kubomoa Kenya kwa mara ya pili mfululizo baada ya kunyakua taji lake la kwanza kabisa kwa kuwalemea 3-0 (25-22, 25-19, 29-17) jijini Yaounde mwaka 2015.

Nyota Christelle Nana amenukuliwa na vyombo vya Cameron akisema, “Kenya ni taifa kubwa la voliboli. Ni mojawapo ya timu kali barani Afrika na itakuwa mechi ngumu zaidi kuliko dhidi ya Algeria, lakini tunajua tunachostahili kufanya na tutajitolea kwa dhati kushinda Kenya.”

Naye Laetitia Moma alisema, “Kila mechi ije inavyokuja. Tutachukulia kila mechi kwa uzito. Kwa hakika, tutajitolea kikamilifu. Ukilinganisha Kenya na Algeria utaona hakuna cha kulinganisha kwa hivyo lazima tuimarishe mchezo wetu.”

Kuepuka wenyeji

Mshindi kati ya Kenya na Cameroon ataepuka kukutana na wenyeji Misri katika nusu-fainali hapo Julai 13. Misri inaongoza Kundi A baada ya kulipua Senegal 3-1 Julai 9 na Morocco 3-2 Julai 10.

Mshindi kati ya Morocco na Senegal atamaliza kundi hili katika nafasi ya pili na kumenyana na nambari moja kutoka Kundi A.

 

Ratiba (Julai 11):

Morocco na Senegal (5.00pm), Algeria na Botswana (7.00pm), Kenya na Cameroon (9.00pm).