Michezo

Malkia Strikers yalenga kusumbua Jamhuri ya Dominican

September 21st, 2019 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

TIMU ya Malkia Strikers ya Kenya inalenga kusumbua Jamhuri ya Dominican katika mechi yake ijayo ya Kombe la Dunia la voliboli ya wanawake linaloendelea nchini Japan.

Katika mahojiano mabingwa hao wa michezo ya Afrika walipowasili mjini Sapporo baada ya kusafiri kilomita 1,365 kutoka mjini Hamamatsu kwa mechi zaidi, kocha mkuu wa klabu ya Kenya Prisons, Josp Barasa amesema, “Tulifika vizuri na hata tumefanya mazoezi. Tutaendelea na mazoezi kesho asubuhi na jioni.”

Barasa, ambaye ni mmoja wa makocha wasaidizi wa Malkia Strikers, amekiri kuwa Dominican ni timu kali iliojaa wachezaji warefu.

Hata hivyo, anaamini wakijipanga vizuri wanaweza kuisumbua. “Tunapanga kucheza mechi ya kasi ya juu. Naamini Dominican ni timu tunayoweza kusumbua tukifaulu kufanya hivi pamoja na kuimarisha kupokea mipira.”

Timu ya Kenya, ambayo iko chini ya uongozi wa kocha Paul Bitok, bado inatafuta ushindi wake wa kwanza.

Mechi dhidi ya Jamhuri ya Dominican, ambayo itasakatwa Septemba 22, ilitanguliwa na vichapo vya seti 3-0 dhidi ya Marekani (25-14, 25-20, 25-14), Uholanzi (25-12, 25-19, 25-17), Serbia (25-13, 25-11, 25-17), Brazil (25-20, 25-17, 25-14) na Argentina (25-14, 25-19, 25-15).

Kwa sasa, Kenya iko mkiani katika nafasi ya 12 bila alama nao mabingwa wa Afrika, Cameroon, walipata alama moja walipotoa Dominican kijasho kabla ya kupoteza kwa seti 3-2 (25-17, 25-15, 23-25, 28-30, 15-10).

Baada ya Dominican, Kenya italimana na Japan (Septemba 23), China (Septemba 24), Korea Kusini (Septemba 27), Urusi (Septemba 28) na kukamilisha kampeni dhidi ya Cameroon (Septemba 29).

Kuhusu maisha nchini Japan, Barasa alisema wanafurahia wali kwa nyama ya ng’ombe, ingawa akakiri kuwa kama Wakenya, wanakosa sana ugali kwa sukumawiki.