Michezo

Malkia Strikers yamulika Kombe la Dunia baada ya kushinda African Games

August 31st, 2019 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

BAADA ya kupiga mahasimu wake wakuu Cameroon mara mbili ikitwaa taji la voliboli ya akina dada kwenye michezo ya Afrika (African Games) nchini Morocco, Malkia Strikers sasa inaelekeza macho yake kwa Kombe la Dunia litakalofanyika baina ya Septemba 14-29, 2019, nchini Japan.

Malkia ilichabanga mabingwa hao wa Kombe la Afrika 3-1 (Agosti 24) na Senegal 3-0 (Agosti 26) katika mechi za Kundi B, ikalima Nigeria 3-0 (Agosti 28) katika nusu-fainali kabla ya kubeba taji kwa kudhihirisha ubabe wake dhidi ya Wakamerun tena 3-1 katika fainali mnamo Agosti 30 usiku jijini Rabat.

Kenya, ambayo sasa inajivunia mataji matano ya wanawake ya African Games (1991, 1995, 1999, 2015 & 2019), pamoja na Cameroon zitawakilisha Bara Afrika katika Kombe la Dunia.

Malkia Strikers ya kocha Paul Bitok itamenyana na Marekani (Septemba 14), Uholanzi (Septemba 15), Serbia (Septemba 16), Brazil (Septemba 18) na Argentina (Septemba 19) mjini Hamamatsu. Itaelekea mjini Sapporo kupepetana na Jamhuri ya Dominican (Septemba 22), Japan (Septemba 23) na Uchina (Septemba 24).

Warembo wa Bitok kisha watazuru mji wa Osaka kuvaana na Korea (Septemba 27), Urusi (Septemba 28) na kukamilisha kampeni yao dhidi ya Cameroon (Septemba 29).

Kenya inashiriki kombe hili kwa mara ya sita baada ya kumaliza makala ya mwaka 1991, 2007 na 2011 katika nafasi ya 12 (mkiani), 1995 katika nafasi ya 11 juu ya Misri iliyovuta mkia, na katika nafasi ya 10 kati ya washiriki 12 mwaka 2015. Jumla ya timu 20 zitawania taji.