Michezo

Malkia Strikers yatua Uganda baada ya nuhusi ya kusubiri tiketi

May 18th, 2019 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

TIMU ya voliboli ya wanawake ya Kenya hatimaye imetua nchini Uganda kwa michuano ya Ukanda wa Tano ya kufuzu kushiriki mashindano ya All-African itakayofanyika Mei 19-21, 2019.

Malkia Strikers haikusafiri jinsi ilivyopangwa kutoka jijini Nairobi siku ya Ijumaa asubuhi ikisubiri tiketi kutoka kwa Wizara ya Michezo.

Taarifa kutoka kambi ya mabingwa hawa wa Afrika ilisema kwamba hawajui kama watasafiri hadi jijini Kampala kwa kutumia ndege ama basi “kwa sababu bado wanasubiri wizara kuwapa tiketi”, ingawa wana matumaini ya kusafiri Jumamosi.

Sasa, timu hiyo ambayo itafungua kampeni dhidi ya Rwanda hapo Mei 19, imethibitisha ilisafiri saa mbili na nusu asubuhi mapema Jumamosi na kutua katika uwanja wa ndege wa Entebbe nchini Uganda saa tatu na dakika arobaini asubuhi.

“Tumefika salama salamini katika uwanja wa ndege wa Entebbe tukitumia ndege ya kampuni ya Kenya Airways,” aliandika mmoja wa makocha wa timu hiyo Josp Barasa katika ukurasa wake wa Facebook.

Mshindi wa Ukanda wa Tano ataingia mashindano ya All-African moja kwa moja. Mashindano hayo ya Afrika yataandaliwa mjini Rabat nchini Morocco kutoka Agosti 19-31, 2019.

Ratiba ya mchujo wa wanawake:

Mei 19

Ethiopia na Uganda

Kenya na Rwanda

 Mei 20

Uganda na Rwanda

Ethiopia na Kenya

Mei 21

Kenya na Uganda

Rwanda na Ethiopia