Malkia Strikers yaungana na Cameroon nusu-fainali ya voliboli Afrika

Na AGNES MAKHANDIA

TIMU ya taifa ya voliboli ya kinadada ya Kenya imefuzu kushiriki nusu-fainali ya Kombe la Afrika kwa mara ya sita mfululizo jijini Kigali nchini Rwanda mnamo Septemba 15.

Malkia Strikers, ambayo ilizoa mataji ya 2011, 2013 na 2015 na kuridhika na medali ya fedha baada ya kupoteza dhidi ya Cameroon katika fainali ya 2017 na 2019, wamelipua Tunisia kwa seti 3-0 za alama 25-20, 25-19, 25-21.

Kocha Paul Bitok alifanyia kikosi kilichopoteza mechi ya kwanza 3-0 dhidi ya Cameroon.

Aliamua kuanzisha seta Esther Mutinda badala ya Joy Lusenaka huku Tunisia ikianza vyema mchuano huo kwa kuongoza 8-5 katika mapumziko ya kwanza.

Bitok kisha alipumzisha Pamela Masaisai na kujaza nafasi yake na mzoefu Mercy Moim na badiliko hilo likaanza kuzaa matunda wakati Kenya ilipunguza mwanya hadi 8-10.

Kenya ilisawazisha 10-10 kabla ya Mutinda, Gladys Ekaru na Leonida Kasaya kushirikiana vyema kuweka Malkia Strikers kifua mbele 13-10 na kuenda mapumziko ya pili 16-13 juu.

Makosa kadhaa upande wa Tunisia yaliwezesha Kenya kufungua pengo la alama tano kabla ya kunyakua seti hiyo kwa alama 25-20.

Kenya ilidhibiti seti ya pili, ikiongoza mapumziko ya kwanza 8-5 na ya pili 16-11.

Tunisia ilitatizika kuwazima Sharon Chepchumba, Moim na Ekaru kabla ya Kenya kutia seti hiyo kapuni kwa alama 25-19.

Kenya ilitolewa kijasho chembamba katika seti ya tatu ikiongoza pembamba 8-7 wakati wa mapumziko ya kwanza huku Bitok akiamua kupumzisha Kasaya na kutumia Masaisai.

Timu hizi zilikuwa sako kwa bako 10-10 kabla ya Kenya kunufaika na makosa ya Tunisia kuchupa uongozini 16-14 wakati wa mapumziko ya pili.

Masaisai, Ekaru na Chepchumba walifunga alama zilizosaidia Kenya kuongoza 22-19 kabla ya timu hiyo kukamilisha kazi kwa kutwaa seti hiyo 25-21.

Kenya itapepetana na Burundi katika mechi yake ya mwisho ya Kundi B hapo Septemba 16.

Wakati huo huo, wenyeji Cameroon walivuna ushindi wao wa tatu mfululizo na tiketi ya nusu-fainali kwa kulipua Burundi 3-0 (25-15, 25-14, 25-14). Rwanda wamenyakua tiketi kutoka Kundi A baada ya kuaibisha Nigeria 3-0 na Morocco 3-0.

Wenyeji Rwanda watahitimisha mechi za makundi dhidi ya Senegal mnamo Alhamisi. Aidha, Kenya ilimaliza mashindano ya Afrika ya wanaume katika nafasi ya tisa mnamo Septemba 14.