Habari Mseto

Malkia wa Ohangla Lady Maureen afariki

July 11th, 2020 1 min read

Na CHARLES WASONGA

MALKIA wa nyimbo za jamii ya Luo anayesifika kwa kuimba kwa mtindo wa Ohangla Maureen Achieng’, maarufu kama Lady Maureen, ameaga dunia baada ya kuugua kwa muda mrefu.

Mwanamuziki huyo alifariki usiku wa kuamkia Jumamosi nyumbani kwa binamuye, Bella Akinyi,  katika eneobunge la Uriri, Kaunti ya Migori.

Akinyi ndiye alithibitisha kifo cha msanii huyo ambaye vibao vyake kama vile “Alemo” (Ninasali) na “Wangni Wabiro” (Wakati huu tunakuja) zilihusudiwa zaidi katika janibu za Luo Nyanza.

“Amekuwa akitunzwa nyumbani kwangu baada ya kuondoka hospitali ya Pastor Machage ambako alikuwa amelazwa tangu Februari mwaka huu,” akasema Bi Akinyi.

Maureen alizaliwa mnamo Novemba 22, 1984 katika kata ya Seme Kombewa, Kaunti ya Kisumu.

Kabla ya kifo chake, uvumi ulikuwa umeenea mitandaoni kwamba kafariki hali iliyomfanya mwanamuziki huyo kunarekodi video kuthibitisha kuwa alikuwa angali hai.

Kifo cha Lady Maureen kinajiri mwezi mmoja baada ya mwanamuziki mwingine kutoka Luo Nyanza, Bernard Obonyo, maarufu kama Abenny Jachiga, kufariki.

Siku chache baadaye, mwaanamuziki wa mtindo wa Benga, Eric Omondo Odit, almaarufu Omondi Long Lilo alifariki katika hospitali ya Kaunti Ndogo ya Bondo, Kaunti ya Siaya alikolazwa baada ya kuugua.

Marehemu alikuwa maarufu kwa vibao kama vile, “Goretti, “Okoth Pilot” na “Kong’o Shida” (Pombe huleta matatizo) ambazo zilitingiza anga ya muziki kwa takriban miaka 13.