Malkia wa vita vya masumbwi Achieng’ kulimana na Melissa kutoka Puerto Rico

Malkia wa vita vya masumbwi Achieng’ kulimana na Melissa kutoka Puerto Rico

Na GEOFFREY ANENE

BONDIA Sarah Achieng’ atachapana na Melissa Hernandez kutoka Puerto Rico hapo Oktoba 21 katika jumba la kimataifa la mikutano la KICC jijini Nairobi.

Achieng’ anarejea ulingoni kutetea taji lake la Baraza la Ndondi la Jumuiya ya Madola (CBC) baada ya kuimarisha rekodi yake hadi ushindi 14 na vichapo viwili alipolemea Anisha Basheel kutoka Malawi katika ukumbi wa Charter Hall jijini Nairobi mnamo Oktoba 20, 2021.

Hernandez ana rekodi ya ushindi 23, kupoteza mapigano manane likiwemo la mwisho dhidi ya Muingereza Chantelle Cameron na kutoka sare mawili. Pigano lao litakuwa kubwa siku hiyo.

Mapambano mengine yatakayofanyika kabla ya Achieng’ almaarufu Angel of War, kuvaana na Melissa, ni Nick Mwangi kulimana na Hannock Phiri, Gabriel Ochieng kupepetana na Haidari Mchanjo, Denzel Onyango kukabiliana na Shaban Ally, Adel Motean kurushiana makonde na Abdul Mwaiki, na Ken St.Pierre kuonyeshana ubabe na Dickson Mwakisopile.

Mapigano haya yameidhinishwa na Chama cha Ndondi za Malipo Kenya (KPBC) na kupata udhamini kutoka kwa FITE, Homeboyz, tikiti na Avenue Healthcare.

  • Tags

You can share this post!

Ingwe washikwa na wasiwasi kuhusu udhamini wa Betika

Ingwe wataka Namwamba afufue soka kuanzia mashinani

T L