Habari Mseto

Malori marufuku katika barabara ya Nakuru-Eldoret Moi akizikwa

February 9th, 2020 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

Malori yanayosafirisha mizigo hayataruhusiwa kwenye barabara ya Nairobi kwenda Eldoret Jumanne na Jumatano ili kuepusha msongamano wakati wa mazishi ya aliyekuwa rais wa pili wa Kenya, hayati Daniel Moi, Inspekta Jenerali wa Polisi, Hillary Mutyambai amesema.

Alitangaza kuwa barabara hiyo ni miongoni mwa kadhaa zitakazofungwa Jumanne na Jumatano wakati wa ibada na mazishi ya hayati Mzee Daniel arap Moi.

Kulingana na ratiba aliyotoa, usafiri utavurugwa kwa siku hizi mbili Wakenya watakapokuwa wakitoa heshima za mwisho kwa Mzee Moi.

Bw Mutyambai amepiga marufuku magari makubwa ya kusafirisha bidhaa katika barabara kuu ya Nairobi-Eldoret kuanzia saa sita mchana Februari 11 2020 hadi Februari 12 saa moja jioni.Jijini Nairobi, barabara ya Aerodrome itafungwa Jumanne (Feburuari 11) kuanzia saa 12 asubuhi, ilhali barabara ya Uhuru Highway itafungwa wakati huo huo.

Barabara zingine zitakazoathirika ni Likoni, Bunyala, Valley Road na mzunguko wa barabara ya kuelekea Ikulu (University Way).

Wenye magari na wananchi wameshauriwa kuzingatia sheria za barabara kuepuka mitafaruku na maafisa wa kudumisha usalama barabarani.

“Idadi kubwa ya maafisa wa polisi itapelekwa katika hafla ambapo ibada ya maombi itafanyika kudumisha usalama,” alisema Bw Mutyambai.

Wananchi wameombwa washirikiane na polisi ndipo ibada ya kutoa heshima za mwisho kwa hayati Moi ifanikiwe.

Marais wa nchi kadhaa wanatarajiwa kuhudhuria ibada ya mazishi itakayofanyika katika uwanja wa michezo wa Nyayo Jumanne.