Habari MsetoMashairi

MALUMBANO: Wadigo mbona hatuwaelewi?

March 31st, 2019 3 min read

Wadigo Mnani?

Bismi natanguliza, sijambo la kulipuza,

Walasitaki likuza, wenzetu watushangaza,

Wazidi kutuchukiza, kila uchao wazuza,

Wadigo ndugu mnani, mbona hatuwaelewi?

 

Vita vyenu na Pilau, hakuna anayepinga,

Acheni zenu dharau, na lugha ya kusimanga,

Jaribuni angalau, mtupe yenye muanga,

Wadigo ndugu mnani, mbona hatuwaelewi?

 

Kwa Shamte na Pilau, mwenginewe simuoni,

Awapingao falau, hela nami nionyeni,

Ni Wadigo wasotao, hebu nanyi chunguzeni,

Wadigo ndugu mnani, mbona hatuwaelewi?

 

Na hamna maadili, lugha yenu yakihuni,

Matusi na idhilali, mtungapo mubaini,

Kwa adabu mumefeli, heshima imfukoni,

Wadigo ndugu mnani, mbona hatuwaelewi?

 

Tamati si kikomoni, si uchokozi jamani,

Mambo yenu ukumbini, yatuudhi tambueni,

Hebu nanyi rekebisheni, lahaula mswalieni

Wandigo ndugu mnani, mbona hatuwaelewi?

Soudy Podos (Tall Guy)

Dukuduku La Rohoni

Bin Sudi Farm

Ganda, Malindi 0714991991

 

Muigizi waigiza, wasia na utetezi,

Chatu anza kuhimiza, digoni wishe ulozi,

Ushirikina wahenza, maendeleo na kazi,

Marigiza humalizi,kasoro unazosaza.

 

Digoni nakueleza, ni makao ya ajizi,

Si uvumi nasambaza, zamani nili mkazi,

Zigo la kuleemaza, li kule haliliwazi,

Marigiza humalizi, kasoro unazosaza.

 

Neno hili Marigiza, “maliza” na humalizi,

Udaku unaukuza, kwa ulimi wa uchizi,

Usojuwa watangaza, kuuzia wanunuzi,

Marigiza humalizi, kasoro unazosaza.

 

Jahim yawakonyeza, waongowa wa udokezi,

Yaso kweli waeneza, jehanamu hubarizi,

Domokaya pulikiza, nikwambalo umaizi,

Marigiza humalizi, kasoro unazosaza.

 

Ulumbi hutauweza, ewe mjipendekezi,

Utajuta kupuuza, ujenzi pasi ujuzi,

Unapojenga uliza, ilipo ile timazi,

Marigiza humalizi, kasoro unazosaza.

 

Jenga kuta ukiwaza, kwa kanuni fatilizi,

Bongo lako elekeza, siyo tu kuchapa kazi,

Myanya itajitokeza, poromoko si hirizi,

Marigiza humalizi, kasoro unazosaza.

 

Zana zako zakubeza, hino ghazi huiwezi,

Fyata haitatuweza, na vijiwe tangulizi,

Vitwaye twakwelekeza, karushie sisimizi,

Marigiza humalizi, kasoro unazosaza.

Wilson Ndung’u

“Mjoli wa Shekinah”

KITALE

 

Jitu lisilo akili, mtashinda mukisema,

Hakanyiki bahaluli, Ba’Shaha bee wa Tsuma,

Kule aswani hoteli, na kwa maulidi juma,

Azidi kushuka nyuma, kwa mahaba ya shamte.

 

Falau sizile dili, za shamte mkauma,

Kosti basi merali, hangeandikwa mgema,

Leo anyeta hamali, atukana Maulana,

Abwambwarishe na nyuma, kwa mahaba ya shamte.

 

Mikanzu na suruwali, kofiya badi karama,

Kujifunza amswahili, majastiki senema,

Mbona kisauni nduli, ulikitwa kishurama?

Zarambo mshuka nyuma, kwa mahaba ya shamte.

 

Chang’aabiri jingili, mtsunga kotso na kima,

Walumbani baradhuli, mwa waungwana khashima,

Jizi gawadi tapeli, wewe na huyo mwangima,

Atele ashuka nyuma, kwa mahaba ya shamte.

 

Sikizani maliwali, hawa si watu si nyama,

Bila Shamte juhali, babu Shaha mduruma,

Hanyi hali na halali, hadi chanda cha karama,

Mpaka ashuke nyuma, kwa mahaba ya shamte.

 

Kutwa majuha wawili, mwa mashebe kulalama,

Hutopata sampuli, mokowe hadi mrima,

Wakishateuka wali, hunusana mataruma,

Mashallahu ana nyuma,kwa mahaba ya shamte.

 

“Ustadhshtua”

AL HABIB MALIK ABDU ALI DHUDHU

Mkubwa Wa Hizo

Mkanyageni, Mombasa.

 

Wilsoni kula pensheni, situpandishe mizuka,

Wajidai kanisani, kibanda umekiweka,

Wategea ihisani, ili upate sadaka,

Wilsoni babaluka, chuma chako kimotoni.

 

Wewe hapa kama nani, siniwache nikacheka,

Hapa ulilumba nini, Kiswahili cha mashaka,

Wajidai ukuhani, kasisi wa kubandika,

Kitale atambulika,Sudi Podo namba wani

 

Hapa pataka kuhani, mwenye kujua lahaka,

Sio huyu mzayuni, wakubadili nyaraka,

Yeye na yule muhuni, wa Takaungu mruka,

Na wakome kukomeka, wasituletee utani.

 

Wakatabahu ilani, Mbogholi nakumulika,

Nani kakupa liseni, hapano kubobojoka,

Ba Shamte mlayuni, na huyo karubandika,

Wote hawajanifika, hata nusu katwaani,

M.M HASSAN

“Ustadh Kigogo”

Al- Walydan Shop

Bombolulu-Mombasa.

 

Nashangaa waandazi, kutwita msaragambo,

Na kupiga ubazazi, eti tuje kuna jambo,

Linataka utatuzi, wa kulifumbua fumbo,

Katika hiki kiwambo, mmetwitani wajuzi?

 

Kwa kusikia mlunzi, nilitinga hadi bombo,

Nikatwaa na muanzi, nikashika na wimbombo,

Nikajihami kwa kurunzi, ni tayari kwa vikumbo,

Katika hiki kiwambo, mmetwitani wajuzi?

 

Nikacha na zangu kazi, nikaja tuimbe nyimbo,

Kumbe ya huku ufyozi, hakuna lenye ulimbo,

Tungo zote simulizi, za watunzi wa kitambo,

Katika hiki kiwambo, mmetwitani wajuzi?

 

Nilidhani kuna ngizi, ama kunga zenye tambo,

Za kututoa ajizi, na tuwe wanamgambo,

Kumbe huku mashauzi, ndio yenu majigambo,

Katika hiki kiwambo, mmetwitani wajuzi?

 

Kusifiana watunzi, kwangu mie si diambo,

Ila kwa lipi la enzi, walilotia urembo,

Si haya yenu manyonzi, kambi kuitia shombo,

Katika hiki kiwambo, mmetwitani wajuzi?

 

Kwa huo wenu ujuzi, tunahitaji vifimbo,

Vilivyo na mwandamizi, na ufupi kwenye umbo,

Sio hizi tukanizi, na tungo zenye mang’ombo,

Katika hiki kiwambo, mmetwitani wajuzi?

 

Hoja ni jambo azizi, na muhimu kwa malumbo,

Zinaleta upendezi, na upevu kwenye mambo,

Hizi zenu gozigozi, naondoka nenda ng’ambo,

Katika hiki kiwambo, mmetwitani wajuzi?

Ismail Bakari

(Swila Mchiriza Sumu)

NAIROBI