Malumbano ya Sonko, Haji yazidi kutokota

Malumbano ya Sonko, Haji yazidi kutokota

NA WINNIE ATIENO

MVUTANO kati ya gavana wa zamani wa Nairobi, Bw Mike Sonko, na Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma, Bw Noordin Haji, umeibuka upya ikiwa mwanasiasa huyo anastahili kuwania kiti cha kisiasa.

Bw Haji ameshikilia msimamo wake kwamba, wanasiasa waliotimuliwa mamlakani kwa sababu za ukiukaji wa sheria, na wale wanaokabiliwa na kesi mahakamani, hawafai kukubaliwa kuwania viti tena uchaguzini.

Kesi kadha zimewasilishwa mahakamani kutaka Bw Sonko na aliyekuwa gavana wa Kiambu, Bw Ferdinand Waititu, wasiidhinishwe na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), kuwania viti katika uchaguzi wa Agosti.Wawili hao walibanduliwa mamlakani kwa makosa ya ufisadi na utovu wa maadili.

“Kama mwendeshaji mashtaka, maoni yangu ni kuwa gavana au mbunge ambaye aling’atuliwa mamlakani na bunge atakuwa amevunja sheria ikiwa atawania kiti cha siasa. Si Bw Sonko peke yake bali wote ambao wamebanduliwa mamlakani lazima wafahamu sheria lazima ifuatwe,” alisema Bw Haji.

Kulingana naye, si sawa kwa mwanasiasa kubanduliwa kaunti moja kwenda kuwania kiti cha siasa kwingine.

“Si sawa kwenda kaunti nyingine kujaribu bahati yako, hili ni suala tunaliangalia kwa karibu kuhakikisha sheria inafuatwa,” alisema.

Awali, Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), ilisema wanasiasa aina hiyo hawaezi kuzuiwa kuwania viti ikiwa wamewasilisha rufaa dhidi ya maamuzi ya kuwabandua mamlakani.

Mapema wiki hii, Mahakama ya Eldoret iliamua kuwasilisha kesi ya kupinga uwaniaji wa Bw Sonko na Bw Waititu kwa Jaji Mkuu ili kutoa mwelekeo wa kuendesha kesi hizo kwa dharura.

Hata hivyo, akianza kufanya kampeni za nyumba hadi nyumba Mombasa, Bw Sonko alisema hatishwi wala kubabaishwa na mtu yeyote anayepinga azma yake kuwania urithi wa kiti cha Gavana Hassan Joho kupitia Chama cha Wiper.

“Hawanitishi wala kunibabaisha. Leo nilikuwa maskan hadi maskan, lango hadi lango kuanzia Old Town, Majengo, ofisi ya Kanu, Mvita na Burnley,” alisema Bw Sonko jana Jumatano.

Mbali na kutangaza rasmi azma yake Mombasa takriban wiki mbili zilizopita, Bw Sonko hajafanya mikutano ya hadhara ingawa kura za maoni zinaonyesha ashajizolea umaarufu kwani kuna pengo dogo kati yake na Mbunge wa Mvita, Bw Abdulswamad Nassir wa Chama cha ODM.

Bw Sonko ambaye alimchagua mbunge wa Kisauni, Bw Ali Mbogo kuwa mgombea mwenza wake, ameonekana kulenga sana kuanza kujipigia debe katika mitaa ya wakazi wenye mapato madogo.

Bw Mbogo alisema licha ya pingamizi tele wanazopitia, anaamini ushirikiano wake na Bw Sonko utawapa ushindi.

Mapema wiki hii, ilifichuka maafisa wa polisi walianza kumchunguza mbunge huyo kwa madai ya uchochezi.

“Sisi tunaendeleza siasa ya maendeleo, hatuna ukabila wala dini, tunataka sote tufaidike. Agosti 9, tutanyakua uongozi, tusiwe na wasiwasi wala shaka moyoni. Nitapigana vita na mabwanyenye wa Mombasa na sitachoka,” alisema Bw Mbogo.

Mbali na Bw Haji, mkuu wa Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC), Bw Twalib Mbarak, pia alisisitiza wanasiasa waliotimuliwa hawastahili kuwania viti upya.

Hivi majuzi, Idara ya Mashtaka ya Umma ilisimamisha kesi za wanasiasa hasa zinazohusu madai ya ufisadi hadi wakati Uchaguzi Mkuu utakapokamilika.

  • Tags

You can share this post!

NDIVYO SIVYO: Neno ‘mgombea-mwenza’ na mitego yake...

Jumla ya watu 55 wanataka kuwania urais

T L