Habari Mseto

Mama afariki baada ya kubugia pombe ya mumewe

September 7th, 2018 1 min read

NA KNA

MWANAMKE wa miaka 36 aliaga dunia Ijumaa, baada ya kutuhumiwa kubugia pombe haramu kutoka nchi jirani iliyokuwa ya mumewe, katika Kaunti ya Siaya.

Bi Grace Hellen Anyango aliaga dunia alipokuwa akikimbizwa katika hospitali ya rufaa ya Siaya na mumewe, baada ya kumpata akigaagaa sakafuni huku kando yake pakiwa na mifuko ya pombe aina ya ‘Simba Waragi’, pombe haramu inayoaminika kutoka Uganda.

Kulingana na naibu wa chifu wa kata ndogo ya Mulaha Marcelus Murunga, kisa hicho kilitokea kijiji cha Rae A ambapo mwanamke huyo alikuwa akiendesha biashara ya kioski cha vyakula.

“Bw Chrispin Owino alikuwa ameondoka na aliporejea alimpata mkewe sakafuni huku akiwa amepoteza fahamu.”

Mwili wa marehemu ulipelekwa katika hifadhi ya maiti ya hospitali ya rufaa ya kaunti, ukisubiri upasuaji.

Aliwaonya wakazi kuhusiana na kutumia pombe haramu, akisema watakaopatikana wakiuza ama kunywa watakamatwa na kufikishwa kortini.

Alisema hii si mara ya kwanza kwa wanawake na vijana kupoteza maisha yao kutokana na unywaji wa pombe haramu.