Habari Mseto

Mama ajiteketeza na watoto wake nyumbani

December 11th, 2018 1 min read

Na Rushdie Oudia

WAKAZI wa eneo la Otonglo, Kaunti ya Kisumu, walisikitishwa na kisa ambapo mwanamke alijiua pamoja na watoto wake wawili.

Mwanamke huyo aliwasha moto na kuteketeza nyumba yale walipokuwa ndani na watoto wake.

Chifu wa eneo hilo, Bw Simon Orwa, jana alisema inaaminika kisa hicho kilitokea baada ya mzozo wa kinyumbani kati ya mwanamke huyo na mume wake ambaye hakuwa nyumbani wakati huo.

Ilisemekana mume wake hufanya kazi Eldoret.

Kulingana na jirani aliyeshuhudia mkasa huo, mwanamke huyo aliyetambuliwa kama Rukia Anyango Wamboga, 26, alirejea nyumbani akiwa amebeba mtungi wenye petroli aliokuwa amenunua katika kituo cha mafuta kilicho karibu.

“Alikuwa amebeba petroli lakini wakati huo singejua ni nini kilichokuwa ndani ya mtungi aliobeba. Alipofika nyumbani aliita watoto wake wawili akafunga mlango kwa ndani,” alieleza jirani huyo.

Muda mfupi baadaye, jirani huyo alisema aliona mwanga mkubwa na moshi kutoka ndani ya nyumba hiyo.

Alipiga ukele kuitisha usaidizi kutoka kwa majirani wengine lakini kwa bahati mbaya hawangeokoa waliokuwa ndani ya nyumba wala mali yoyote kwani kila kitu kiliteketea.

Watoto hao wawili walitambuliwa kama Shirleen, 6, na Asman, 2.

“Alikuwa ameniambia kuhusu matatizo yanayowakumba nyumbani nikamwambia asimame imara. Nimehuzunishwa sana na kisa hiki,” mamake mwnamke huyo, Bi Sarah Wamboga, alisema huku akilia.

Alikuwa amekuja hapo kwa haraka kutoka Eldoret punde tu alipofahamishwa kuhusu kisa hicho.