Habari Mseto

Mama akiri kumuuza mtoto wake kwa Sh1,200

September 12th, 2018 1 min read

Na MERCY KOSKEY

MWANAMKE wa miaka 35 Jumatano alikiri kosa la kujaribu kumuuza mwanawe kwa Sh1,200 alipofikishwa kortini.

Bi Ann Wangui Maina alifikishwa mbele ya Hakimu Mkuu Joe Omido na kushtakiwa kwa ulanguzi wa binadamu, baada ya kutuhumiwa kumuuza mtoto wake wa wiki mbili Jumanne.

Mshtakiwa alikamatwa siku hiyo katika Hospitali ya Rufaa ya Nakuru, alipokuwa akitaka kumuuzia Bi Dorcas Nanjala mwanawe wa kike, baada ya Bi Nanjala kumpoteza mtoto wake alipojifungua.

Kulingana na mashtaka, Bi Wangui alipokea Sh1,200 kutoka kwa Bi Nanjala kwa nia ya kumuuzia mtoto huyo na hivyo kumnyima mtoto mwenyewe haki ya ulezi wa mama.

Korti ilielezwa kuwa mshukiwa alitenda kosa hilo Septemba 11 katika hospitali hiyo ya Nakuru Level Five ambapo alikuwa amemweleza Bi Nanjala afike siku ya Jumatatu kabla ya saa tano ili amchukue mtoto.

Korti aidha ilielezwa kuwa mshukiwa alimtaka Bi Nanjala kufika hospitalini na mavazi ya kumvisha mtoto huyo.

Lakini Bi Nanjala alipiga ripoti kwenye kituo cha polisi cha Central mjini Nakuru na akaandamana na askari wawili wakiwa katika mavazi ya kawaida, akiwa na bidhaa alizokua ameagizwa apeleke hospitalini.

“Alisema pesa hizo Sh1,200 zilikuwa za kugharamia vifaa na nguo alizomnunulia mtoto huyo kwa kipindi cha wiki tatu alizokuwa naye,” akasema Bi Nanjala siku alipokamatwa mshukiwa.

Walipofika alikamatwa na askari hao.

Mahakama iliamuru mshukiwa azidi kuzuiliwa rumande hadi atakaporejeshwa kortini tena leo kuhukumiwa.