Habari Mseto

Mama akiri kuua mtoto kwa kumtupa mgodini kwa sababu ya ugumu wa maisha

June 14th, 2024 1 min read

NA JUDY CHERONO

MWANAMKE katika mahakama ya Kisumu amekiri kumuua mtoto wake wa miaka mitatu kwa kumtupa kwenye mgodi.

Mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 23, alisimulia mahakama jinsi alivyomtupa mtoto wake kwenye mgodi uliotelekezwa, akidai kwamba hangeweza kumtunza kutokana na mapato yake duni.

Alishtakiwa kwa kutekeleza mauaji hayo mnamo Mei 7, 2023, Kanyakwar, Kaunti ya Kisumu.

Alipatikana akiwa sawa kiakili kujibu mashtaka baada ya kufanyiwa ukaguzi wa akili katika Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Jaramogi Oginga Odinga (JOOTR) mnamo Mei, 23, 2023.

“Naitwa Margaret Achieng, nilikuwa naishi Kondele, na nilikuwa nafanya kazi hotelini. Reagan Otieno alikuwa mwanangu.  Mpenzi wangu aliniacha nilipopata ujauzito mwaka wa 2021. Nilikuwa nikifanya kazi duni ili kumtunza,” alieleza korti.

Aliongeza, “Nilipopata kazi katika hoteli hiyo, nilimchukua mwanangu na kumpeleka kuishi na mjomba wangu katika vitongoji duni vya Obunga.

“Ila kuna mjomba wangu mwingine aliyekuja na kunieleza kuwa mwanangu anateseka. Kwa kuwa nina mapato duni, singeweza kukidhi mahitaji yake,” alisimulia.