Habari Mseto

Mama alinunulia wanawe nguo za mazishi kabla awaue

June 29th, 2020 1 min read

Na MACHARIA MWANGI

IMEBAINIKA kuwa mwanamke aliyekamatwa na polisi kwa kuua watoto wake wanne mjini Naivasha, Kaunti ya Nakuru alikuwa amearifu familia yake na mwana wake mkubwa kuhusu mpango huo wa kikatili.

Mahojiano na jamaa zake yamefichua kuwa mshukiwa huyo alikuwa amenunua nguo mpya za kuzika watoto wake na akaandaa sehemu ambapo alitaka wazikwe.

Katika barua aliyomwandikia mtoto wake wa kiume ambaye ni mwanafunzi wa chuo kikuu, mwanamke huyo alikuwa amelalamikia ugumu wa maisha uliomfanya kushindwa kulipa kodi ya nyumba tangu Aprili.

“Ninajua ninastahili kuwa jela. Nina hakika nitatumikia maisha yangu yote gerezani lakini niko tayari kwa hilo,” barua hiyo ikasema.

Kando na hayo, alimlaumu mpenzi wake kwa kumsaliti. Alimwonya mtoto huyo dhidi ya kushirikiana na mpenzi huyo wake wa zamani.

Wakati wa mkasa, alikuwa na watoto wake wanne nyumbani kwa kuwa wawili hawakuwepo.

Mbali na barua hiyo kwa mvulana huyo, nduguye mdogo Bw Jackson Kimotho, alieleza jinsi dadake alivyotoa vidokezo kuhusu mipango yake kwa familia. Alisema mshukiwa aliweka picha za watoto hao katika mtandao wa kijamii wa WhatsApp wa familia hiyo mnamo Jumamosi, mwendo wa saa nane mchana.

Inaaminika watoto hao wanne walinyweshwa sumu Ijumaa, kisha wakanyongwa.

“Alikuwa anataka maoni yetu kuhusu watoto wake. Mmoja wetu akasema walikuwa wanapendeza,” akaeleza.

Alianza kuandika mambo ya kushangaza wakati huo huo kama vile: “Kaeni kimya kwa muda ili kuwapa watoto wangu heshima za mwisho.”

Kisha akaandika: “Sielewi, wamekufa. Nimewaua.” Baadaye, aliweka picha ya zamani ikiwa na maandishi: “Betty muuaji. Mwombeeni roho yake iwe na amani humu duniani.”

Msimamizi wa kikundi hicho cha WhatsApp alimwondoa mara moja, huku familia ikianza kuingiwa na wasiwasi. Alipotambua ameondolewa katika kikundi hicho, mshukiwa alimpigia simu Bw Kimotho akimtaka aandamane na polisi hadi nyumbani kwake.