Kimataifa

Mama aliyedai mumewe ana 'jembe ndogo' taabani

February 21st, 2019 1 min read

MASHIRIKA Na PETER MBURU

MWANAMUME ambaye mkewe alimwanika kwenye mitandao ya kijamii kuwa ana ‘jembe ndogo’ sana na kuwa alikataa kufanya mapenzi naye hadi walipooana ili kuficha ukweli huo sasa ametishia kumshtaki mkewe huyo kwa kumchafulia jina na kumuaibisha.

Mwanamke huyo alitumia mtandao wa Reddit kufungua moyo wake kuwa mumewe waliyeoana majuzi alimhadaa kuwa wasubiri hadi watakapofunga ndoa ili kufanya ngono, japo baada ya harusi akabaini kuwa mwanamume huyo ana kiungo cha uume kidogo kupita kiasi.

Alisema alibaini hivyo walipokuwa wakisherehekea fungate, ambapo walipotaka kufanya mapenzi aligundua kuwa uume wa mpenzi wake ulikuwa mdogo ajabu. Hata hivyo, hakumtaja mumewe.

Lakini sasa baada ya ujumbe huo kusambaa sana kwenye mtandao wa Reddit, mumewe alibaini kuwa amekuwa akizungumziwa mitandaoni na sasa ametishia kufika kortini.

Hii ni baada ya ujumbe wa mwanamke huyo kuvuta maelfu ya majibu kutoka kwa watu, na kuchapishwa na mashirika kadha ya habari Uingereza.

Mwanamke huyo alirejea kwenye mtandao wa Reddit awali wiki hii, sasa akidai kuwa mumewe anatishia kumtaliki na kumshtaki.

“Mume wangu aliona ujumbe niliotuma na anasema anataka kuniacha na anishtaki. Anasema anawaza kunishtaki kwa kumharibia jina,” akasema.

Alisema kuwa mumewe anasema ni muda tu na jina lake litafahamika kote.

“Aliona ujumbe kupitia rafiki yake wa zamani ambaye anafahamu kuwa ana uume mdogo, ambaye aliona kwenye akaunti yake ya Facebook kuwa alioa. Amekasirika kuwa nilichapisha ujumbe kumhusu,” akachapisha mwanamke huyo.

Alisema kuwa mumewe alikiri kuwa alificha ukweli huo kwani alihofia kuwa angemwacha endapo angefahamu.

“Nilimuuliza wiki iliyopita na akasema kuwa alificha kwani aliogopa ningemwacha ikiwa ningefahamu kabla ya harusi,” akasema.

Watumizi wa mitandao, hata hivyo, walimpa mwanamke huyo moyo kuwa hakukosea kujulisha ulimwengu kuhusu tatizo la mumewe, wakisema hata mwanamume huyo hakufaa kumficha ukweli huo muhimu.