Habari Mseto

Mama aliyemchinja bintiye kuona cha moto

October 15th, 2018 1 min read

Na FRANCIS MUREITHI

POLISI katika kaunti ya Samburu wanamzuilia mwanamke eneo la Baragoi kwa madai ya kuhusika na mauaji ya mtoto wake wa kike mwenye umri wa miaka miwili na kisha kumjeruhi mwingine wa miaka saba.

Kamanda wa Polisi katika kaunti ya Samburu, Bw Alfred Agengo, alisema mshukiwa anazuiliwa katika kituo cha polisi cha Baragoi, na anatarajiwa kufikishwa kortini leo, ili kujibu mashtaka ya mauaji ya mwanawe.

Bw Agengo amedokeza kuwa polisi pia wameanzisha uchunguzi wa kina kubainisha kilichosababisha mshukiwa kumuua mtoto huyo.

Aidha mama huyo mwenye hasira aliwageukia wanawe mnamo siku ya Jumamosi na kuwakata koo na shingo akitumia kisu cha jikoni.

Mumewe Bw Mayan Lorno hakuwepo nyumbani wakati tukio hilo lilipofanyika.

Hata hivyo, Bw Lorno alifichua kuwa mkewe amekuwa akiugua maradhi ya akili katika siku za hivi karibuni na amekuwa akipokea matibabu katika hospitali mjini Baragoi na Maralal.

“Tumeishi vizuri kama mume na mke na licha ya kuwa mke wangu alikuwa na ugonjwa wa akili, alipokea matibabu na kisha kupona. Sielewi kwanini alitekeleza kitendo hicho cha unyama,” akasema Bw Lorno.

Mtoto aliyenusurika kifo yuko mahututi na anapokea matibabu katika hospitali ya kaunti ya Samburu iliyoko mjini Maralal.