Habari Mseto

Mama aliyemlaghai mwenzake mamilioni motoni

August 8th, 2018 2 min read

Na RICHARD MUNGUTI

MKURUGENZI wa Mashtaka ya Umma (DPP) Jumanne aliomba mfanyabiashara aliyemlaghai mwenzake Sh9.9 milioni akidai atamuuzia mafuta ya Petroli azuiliwe kwa muda wa siku tatu.

Kupitia kwa kiongozi wa mashtaka Bi Kajuju Kirimi, DPP alisema polisi hawajakamilisha uchunguzi dhidi ya Bi Caroline Murugi Nthumbi.

Ijapokuwa ombi hilo la DPP lilipinga hakimu aliamuru mshtakiwa azuiliwe kwa siku mbili na kesi itajwe Agosti 10.

“Mshtakiwa atazuiliwa kwa siku mbili. Zikikamilika mshtakiwa atalipa dhamana ya Sh1milioni pesa tasilimu,” aliagiza hakimu mkuu katika mahakama ya Milimani Bw Francis Andayi.

“Maafisa wa polisi wanahitaji muda wa siku tatu kumhoji mshtakiwa na kupokea ushahidi zaidi kumuhusu,” kiongozi wa mashtaja alimweleza  Bw Andayi.

Mahakama ilifahamishwa kuwa polisi wanataka kufika katika makazi ya mshtakiwa kuyasaka kupata ushahidi muhimu.

Lakini ombi hilo lilipingwa vikali na wakili Danstan Omari aliyesema kuwa “ hakuna afidaviti iliyowasilishwa na afisa anayechunguza kesi dhidi ya Bi Nthumbi akisimulia sababu za kutaka mshtakiwa azuiliwe.”

Bw Omari alisema kuwa ni sheria iliyo wazi kuwa ikiwa mshtakiwa anatakiwa kuhojiwa , polisi wapasa kuwasilisha ushahidi wa kutosha ndipo mahakama itoe maagizo yanayolingana  na ushuhuda uliowasilishwa.

Bw Omari alisema ombi la Bi Kirimi haliwezi kukubalika kwa vile mshtakiwa amesomewa shtaka na kukanusha.

“Naomba mshtakiwa aachiliwe kwa dhamana. Amekanusha shtaka dhidi yake na kilichoko sasa ni apewe dhamana,” alisema Bw Omari.

Shtaka dhidi ya Bi Nthumbi lilikuwa kati ya Oktoba 27 na Novemba 7, 2016 alipokea Sh9,911,000 kutoka kwa Bi Naomi Mwende Akisha akidai alikuwa na uwezo wa kumuuzia mafuta ya Petroli.

Shtaka lilisema kuwa mshtakiwa alijifanya alikuwa na uwezo huo kumbe anandanganya tu.

Hakimu alifahamishwa kuwa kuna kesi nyingine dhidi ya mshtakiwa itakayounganishwa na hili la ulaghai wa Sh9.9milioni.

“Naamuru kesi hizi ziunganishwe ndipo korti iwe na fursa ya kuzingatia madai yote,” aliamuru hakimu mkuu katika mahakama ya Milimani Bw Francis Andayi.

Kiongozi wa mashtaka Bi Kirimi alikabiliwa na wakati mgumu kuhusu kesi hizo mbili kumuhusu mshtakiwa mmoja.

Bi Kirimi alieleza, “Faili moja ilipelekwa kwa hakimu mwingine na nyingine ikawasilishwa mbele yako.”