Kimataifa

Mama ampiga risasi 'fisi' aliyenyemelea mtoto wake

July 11th, 2018 1 min read

Na MASHIRIKA

VIRGINIA, AMERIKA

MWANAMUME aliyesafiri zaidi ya kilomita 13,000 kwenda kumtembelea msichana mdogo mwenye umri wa miaka 14, alipigwa risasi na mamake mtoto huyo.

Mwanamume huyo aliyetambuliwa kama Troy George Skinner, 25, alikuwa amesafiri kutoka nchini New Zealand hadi mjini Virginia, Amerika, kukutana na msichana huyo ambaye walikuwa wakiwasiliana mtandaoni awali.

Mkuu wa polisi wa mtaa wa Goochland ambako tukio hilo lilitendeka, James Agnew, alinukuliwa kusema jamaa huyo alivunja mlango wa nyumba ya kina msichana huyo kisha akajaribu kuingia.

Inaaminika alikuwa na nia mbaya kwani ilibainika alikuwa amenunua karatasi ya gundi na kisu alipowasili Amerika.

Kwa mujibu wa mashirika ya habari, mamake msichana huyo alimwona jamaa akiingia kwa nyumba yake na akaonya kwamba ana bunduki. Alimpiga risasi alipovunja mlango na kumjeruhi shingoni.

Polisi walisema mwanamume huyo atashtakiwa kwa kuvunja nyumba ya wenyewe na kuingia akiwa na silaha na nia ya kutenda uhalifu mkubwa.

-Imekusanywa na Valentine Obara