Dondoo

Mama ampokonya binti dume lenye hela

May 13th, 2018 1 min read

Na BENSON MATHEKA

UTAWALA, NAIROBI

MWANADADA wa hapa aliwashangaza wakazi kwa kumlilia mama yake akome kuchepuka na mpenzi wake.

Kipusa huyo alidai kwamba mama yake, ambaye hajaolewa, alikuwa amempokonya mpenzi wake tunayefahamishwa ni bwanyenye anayemiliki nyumba nyingi za kukodisha jijini Nairobi.

Kulingana na mdokezi, demu alikutana na jamaa huyo katika hafla moja na baada ya kurushiana misitari walianza kutoka.

“Wamekuwa wapenzi kwa muda na hata jamaa amemnunulia demu gari na nyumba anayoishi na mama yake ambaye hajaolewa,” alisema mdokezi.

Jamaa alikuwa akimtembelea demu nyumbani na wakazi wa hapa walikuwa wakimchukulia kuwa mumewe.

“Alikuwa akifika jioni kwa magari tofauti ya kifahari na kuondoka asubuhi,” alisema mdokezi.

Inasemekana hivi majuzi, demu alitoka kazini na marafiki zake na wakaamua kupitia katika kilabu kimoja mtaani hapa kujivinjari kabla ya kuelekea nyumbani.

Katika kilabu hicho alishangaa kumpata mpenzi wake na mama yake wakiketi pembeni wakiendelea kuburudika. “Demu hakuamini kwamba mama yake angeweza kuwa baa na mpenzi wake wakiburudika.

Alitaka kuwavamia lakini marafiki zake wakamshauri asizue kisanga kilabuni. Waliondoka na kumpeleka nyumbani,” alieleza mdokezi.

Penyenye zasema kuwa jamaa aliwasili akimbeba mama ya demu kwenye gari lake wakiwa walevi na kipusa akaanza kumfokea mama.

“Kwa nini unatembea na mpenzi wangu kilabuni kulewa? Hii ni heshima kweli? Mbona unataka kunipokonya mzee wangu mama?” demu aliwaka.

Mama ambaye alikuwa mlevi alimjibu kwa ukali akimwambia kwamba jamaa alikuwa mtu mzima mwenye haki ya kuamua anayetaka kupenda.

“Muulize mwenyewe kanialika. Ni mtu mzima na ana haki ya kujiamulia mambo,” alisema mama.

…WAZO BONZO…