Habari Mseto

Mama anyonga mtoto mwenye umri wa miezi sita na kujiua

May 14th, 2020 1 min read

Na GEORGE MUNENE

WAKAZI wa kijiji cha Mukinduri, Kaunti ya Kirinyaga waliamkia tukio la kushangaza Jumatano mwanamke alipodaiwa kumuua mtoto wake aliyekuwa na umri wa miezi sita na kisha kujiua kwa kujitumbukiza kisimani.

Mwanamke huyo, Purity Kawira aliyekuwa na umri wa miaka 26 alimnyonga mtoto kabla ya kujirusha ndani ya kisima cha futi 70 kilichoko nyumbani kwake.

Ingawa haikuweza kubainika mara moja sababu za kutekeleza kitendo hicho, wakazi wanashuku alichukua hatua hiyo kufuatia mzozo wa kinyumbani.

Mumewe, Bw Paul Gaciani alisema hakuwa nyumbani tukio hilo lilipofanyika.

“Sijui sababu ya mke wangu kuua mtoto na kisha kujiua. Sikuwa karibu wakati huo,” alieleza.

Mmoja wa jamaa wao, Bi Jecinta Wanjiru, 60 alizirai kufuatia kisa hicho.

Afisa wa Kaunti ya Kirinyaga, Bw John Kiama alisema alikuwa miongoni mwa wafanyakazi wa idara ya zimamoto kuwasili hapo.

“Tulikuwa na wakati mgumu kujaribu kutoa mwili wa mama huyo kisimani. Tulifaulu na kuupokeza kwa polisi,” alisema.