Habari Mseto

Mama aokolewa baada ya kuishi mbugani kwa miezi 2

September 27th, 2019 2 min read

Na ANTHONY KITIMO

KULIKUWA na shughuli za kipekee katika kituo cha polisi cha Voi, Kaunti ya Taita-Taveta baada ya mama aliyepatikana katika mbuga hatari ya wanyama ya Tsavo Magharibi kupatanishwa na mwanawe.

Bi Annesita Kageni ambaye aliripotiwa kutoweka kutoka Kaunti ya Tharaka Nthi miezi tisa iliyopita alipatikana katika mbuga hiyo japo akionekana kutatizika kiakili.

Mama huyo wa miaka 48 ameishi katika mbuga hiyo hatari inayofahamika kwa wanyama kama ndovu, simba na nyati kwa zaidi ya miezi miwili kulingana na polisi.

Caroline Kageni, mwanawe Bi Kageni alisema familia na marafiki walipoteza matumaini ya kumpata mamake kwani kwa muda wa miezi tisa wamezunguka sehemu mbali mbali wakimsaka.

“Mama alipotea tarehe 31 mwezi wa Novemba mwaka jana na tangu hapo tumekuwa tukimtafuta bila mafanikio. Ni jambo la furaha kukutana na mamangu siku hii ya leo baada ya polisi kumpata kilomita kadhaa ndani ya mbuga ya wanyama ya Tsavo,” alisema Caroline.

Aliongeza kuwa, simu ya afisa wa polisi aliyopokea siku ya Jumatano kumuarifu kuhusu kupatikana kwa mamake ilikuwa simu ya mwamko mpya katika maisha yake.

“Hatukudhania tutampata mamangu kwani miezi miwili iliyopita tuliambiwa alionekana katika mbuga hiyo ambayo ina wanyama wakali lakini twashukuru Mungu kwa yote aliyotutendea kumpata mamangu mzima,” alisema mwanawe huku akibubujikwa na machozi ya furaha.

Kusifu raia

Afisa mkuu wa polisi eneo la Voi Bernastian Sharry alisema tangu mama huyo kuripotiwa kuonekana eneo la Tsavo wamekuwa macho na akasifu raia ambao wameshirikiana nao kumuokoa mama huyo.

“Mbuga ya wanyama ya Tsavo ni hatari lakini tumekuwa tukiwasiliana na watu mbalimbali ambao wamekuwa wakituarifu mama huyo kila alipoonekana,” alisema Bw Sharry.

Afisa huyo wa polisi alisema mama huyo mara ya kwanza alionekana eneo hilo miezi miwili iliyopita laakini wakati polisi walipofika katika mbuga hiyo alikuwa tayari amepotea.

Katika mbuga hiyo, kumekuwa na visa vingi vya miili kupatikana baada ya kuripotiwa kupotea na kupatikana kwa mama huyo akiwa hai wengi wamekutaja kama maajabu.