Dondoo

Mama apewa kipigo cha mbwa koko kwa kutesa mtoto

March 3rd, 2019 1 min read

Na Ludovick Mbogholi

MAJAONI, MOMBASA

Mama wa hapa alijipata mashakani kwa kumtesa mwanawe wa umri mdogo kwa kumtembeza juani akiwa miguu peku, huku akimsukuma na kumtusi.

Yasemekana akina mama mtaani walikasirishwa na tabia ya mwanamke huyo na kumkemea vikali wakitaka kumwadhibu.

“Unadhani miguu ulipewa ya nini?” mama alisikika akimfokea mtoto aliyekuwa akilia sana kwa kuchomwa na jua.

Kulingana na mdokezi, mtoto alikuwa shuleni na ilisemekana alitoroka akarejea nyumbani.

“Wanawake wenzake walimuona ameshika fimbo huku akimfokea mtoto na kumsukuma. Mtoto alionekana akilia kwa sauti ya juu huku akianguka na kugaagaa chini, mamake akimchapa na kumrushia maneno yasiyo ya heshima,” asema mdaku aliyeshuhudia kisa hiki.

Wanawake walisikia uchungu walipomuona mtoto akichechemea kwa kuchomwa na jua huku mama aliyevaa champali akimkaripia na fimbo mkononi.

“Unamtesa mtoto namna hii, ni wako au ni wa kambo?” walimuuliza kwa hasira. “Mnadhani ni wa nani?” mama aliwajibu huku akimvutavuta.

“Unavyompiga na kumsukuma juani ni kama si wako, hujui uchungu wa kuzaa,” alimkaripia mama aliyemuokoa mtoto asitandikwe zaidi. Yasemekana mwanamke huyo aliwageukia akina mama hao.

“Mnanijua au mnaniona tu nikipitapita hapa, uchungu wa kuzaa unawahusu nini,” aliteta vikali mama huyo.

Maneno makali yaliyotoka vinywani mwa wanawake hao yaliibua patashika kali kwani mama wa mtoto alimrukia mmoja wao na kumchapa kofi na ikawa na sawa na kufungulia nyuki mzingani.

Inasemekana wanawake watano walimrukia na kumtwanga huku wakimkemea.

“Kuzaa unajuwa kulea unashindwa. Tangu lini mtoto akateswa juani, hana viatu unamwambia akazane. Huoni umri wake ni mdogo,” alifokewa huku akichapwa.

“Huyu mwanamke ni kama alimpata mtoto mitaani,” alimaka mama mmoja.