Dondoo

Mama arudi kwao akilia mume hachovyi asali

April 2nd, 2019 1 min read

NA MIRRIAM MUTUNGA

MUKONDE, MBOONI

MAMA wa hapa aliwashangaza wakazi kwa kufunganya virago na kurudi kwa wazazi wake akidai kuwa mumewe alikuwa amemkausha chumbani kwa miezi kadhaa.

Kulingana na mdokezi, mume wa mwanadada huyo hufanya kazi mjini na kila mara akimtembelea mkewe, huwa anarudi siku hiyo ilhali mkewe huwa amemkosa sana.

Katika hali hiyo mkewe alianza kushuku kuwa jamaa hakuwa akimtamani.

Mwanadada alidai kabla ya kupata kazi mjini mumewe alikuwa akimshughulikia vyema chumbani kila usiku.

Alisema alimuacha akisononeka kwenye baridi na hata akimtembelea hakua na wakati wa kulala nyumbani.

Siku ya kioja, jamaa alimtembelea mkewe na kama ilivyokuwa kawaida yake akamuarifu angerudi mjini siku hiyo.

Mkewe alipandwa na hasira na akaanza kumfokea akimlaumu kwa kumtekeleza.

“Inakuwaje sasa ni miezi mitatu imepita na haunifeel hata kidogo? Tangu ulipopata ajira mjini mambo yalibadilika kabisa.Mimi siwezi nikavumilia kuishi maisha ya upweke zaidi ya hapo,” mke wa polo alilalamika.

Jamaa alijitetea na kusema kuwa kazi imekuwa nyingi na ndiyo sababu ya kukosa nafasi ya kuchovya asali.

Alimweleza mkewe kwamba alitaka kuchunga kazi iliyokuwa kuwapa riziki. Hata hivyo, mke wa jamaa alikana maneno hayo na kumwambia anashuku ana mpango wa kando.

“Umetekwa na vipusa wa mjini ukanisahau mimi mkeo hata hautaki kulala nyumbani. Basi kaa na hao, nitaenda kutafuta wa kunishughulikia, ” alisema mwanadada huyo.

Jioni hiyo baada ya jamaa kuondoka kurudi kazini mkewe alichukua kilichokuwa chake na kuondoka akilalamikia tabia ya mumewe.

Hata hivyo, mdokezi wetu hakuweza kubaini hatua ambayo mume aliamua kuchukua baada ya kupata ujumbe kuwa mke kafunganya virago na kurejea kwao.