Habari Mseto

Mama asema polisi wanachunguza kisa cha mtoto wa umri wa miaka 3 kunajisiwa

February 18th, 2020 1 min read

Na LAWRENCE ONGARO

MWANAMKE mmoja wa kijiji cha Kiganjo, Thika, anataka apate haki baada ya mtoto wake mwenye umri wa miaka mitatu kunajisiwa.

Mzazi huyo anasema mtoto wake hupelekwa katika shule ya malezi na gari kila asubuhi, lakini mwishoni mwa wiki mambo yalikuwa tofauti.

Alisema mtoto wake huchukuliwa na gari hadi kituo hicho cha malezi, halafu jioni anarejeshwa nyumbani kama kawaida.

“Wakati aliporejeshwa jioni nilishang’aa kupata ya kwamba alikuwa na tone la damu katika sehemu zake za siri. Baadaye nililazimika kwenda polisi kuandikisha taarifa,” amesema mama huyo.

Amesema alipewa cheti cha P3 ili kwenda nacho hospitali kwa matibabu ya mwanaye, ambaye alionyesha maumivu mengi kutoka sehemu zake za siri.

“Baada ya daktari kumpima ilithibitishwa ya kwamba alikuwa amenajisiwa. Mimi kama mamake mzazi bado ninashindwa kuelewa ni nani hasa anaweza kuwa alitenda unyama huo,” akasikitika mama huyo.

Hata hivyo, msimamizi wa shule hiyo alikataa kuzungumzia jambo hilo baada ya kuhojiwa na mamake mtoto.

Bi Wambui amesema tayari polisi wanaendelea kufanya uchunguzi kamili ili kubaini ukweli wa mambo uko wapi.

Wakazi wa kijiji cha Kiganjo mahali mama huyo anakoishi wamebaki na mshangao wasijue la kusema baada ya mtoto huyo kutendewa unyama huo.

“Mimi mzazi wa mtoto wangu mpendwa ninashindwa kujua ukweli wa mambo jinsi mtoto huyo anaweza akafanyiwa unyama wa aina hiyo,” akasikitika mama huyo.

Hata wazazi walio na wana wao katika shule hiyo wameachwa na mshangao mkubwa wakijiuliza maswali yanayokosa majibu.