Habari Mseto

Mama asukumwa jela miaka 8 kwa kukata nyeti za mumewe

August 21st, 2018 1 min read

Na TITUS OMINDE

MWANAMKE aliyepatikana na hatia ya kujeruhi mume wake sehemu za siri kwa kutumia kisu chenye makali alifungwa jela kwa miaka minane na mahakama moja mjini Eldoret.

Erika Iminza Shihenda 23 alishtakiwa kwa kumsababishia mume wake majeraha katika sehemu yake ya siri kwa kumchanja akitumia kisu chenye makali. Stakabadhi za mahakama zilionyesha kuwa kisa hicho kilitokea katika mtaa wa Huruma mjini Eldoret mnamo usiku wa Mei 22 mwaka huu.

Mahakama iliambiwa kuwa mlalamishi aliamshwa usiku wa manane mwendo wa saa nane kutokana na uchungu ambao alikuwa akihisi katika sehemu ya uume wake kutokana na makali ya kisu. Mshtakiwa alikana mashtaka husika mbele ya hakimu mkuu wa Eldoret Bw Charles Obulutsa.

Akitoa hukumu, Bw Obulutsa alisema mahakama ilishawishiwa kuwa mshtakiwa alipatikna na hatia.

Hakimu alisema kuwa upande wa mashtaka uliridhisha mahakama kubaini kuwa mshtakiwa alikuwa na hatia kwa mujibu wa mashtaka husika.

Mshtakiwa alionekana kuchanganyikiwa pale alipoambiwa ajitetee kabla ya kuhukumiwa kwani badala ya kujitetea aliambia mahakama impunguzie bondi.

“Mlalamishi aliambia korti kuwa alihisi uchungu mkali wakati wa tukio hilo ambapo mke wake alitoroka baada ya kumjeruhi. Mlalamishi alijikokota hadi katika njia ambayo ilikuwa karibu na nyumbani kwake ambapo aliokolewa na Wasamaria wema ambao walimpelka katika hospitali ya Huruma kwa matibabu,” alisema hakimu huku aktoa hukumu.