Mama Ida tumaini tele Raila atashinda kura

Mama Ida tumaini tele Raila atashinda kura

Na VICTOR RABALLA

MAMA Ida Odinga, mkewe Kinara wa ODM Raila Odinga amesema kuwa uchaguzi mkuu wa 2022 ndio utatoa nafasi bora zaidi kwa waziri huyo mkuu wa zamani kushinda kiti cha Urais.

Hii ni licha ya kuwa Bw Odinga amekuwa akipokea upinzani mkali kutoka kwa Naibu Rais Dkt William Ruto ambaye pia analenga kurithi kiti hicho baada ya Rais Uhuru Kenyatta kustaafu siasa mwaka ujao.Akizungumza katika Kaunti ya Siaya mnamo Jumatano, Bi Odinga alisema kuwa serikali ya mumewe itajali sana maslahi ya vijana kwa kuwapa nafasi nyingi za ajira na pia kuwashirikisha katika masuala ya uongozi.

“Lazima tuwe watulivu na kudumisha amani ili tuvutie uungwaji mkono kutoka jamii nyingine,” akasema Bi Odinga huku akiwataka wafuasi wa ODM wajitokeze kwa wingi kumpigia kura mumewe ili aingie mamlakani.“Tulianza safari ya kuelekea Canaan na sasa imebakia kilomita chache tufike.

Hatutaki mtu asalie nyuma tunapojitihadi kufika nchi ya ahadi ambayo imejaaliwa mema,” alisema Bi Odinga, ambaye amekuwa akimvumisha sana mumewe kwenye kampeni za kuelekea kura ya 2022.Naibu Waziri wa Jinsia na Huduma za Kijamii Rachel Shebesh naye alikariri kuwa eneo la Mlima Kenya litamuunga mkono mwaniaji ambaye ataungwa mkono na Rais Uhuru Kenyatta.

Bi Shebesh alisema kuwa ni Rais Kenyatta pekee ambaye ana uwezo wa kutoa mwelekeo kuhusu nani anayefaa kuongoza nchi baada ya hatamu yake kukamilika.Vilevile, Bi Shebesh alimkashifu Dkt Ruto na wafuasi wake kwa kurejelea Bw Odinga kama mradi wa serikali, akisema si vibaya kwa Rais ambaye yupo mamlakani kumuunga mkono au kumteua mrithi wake.

“Ni aibu kuwa baadhi ya watu wameanza kujipiga kifua jinsi ambavyo walikuwa na watu wa Mlima Kenya kwenye mifuko yao. Hakuna mtu anafaa kujidai kuwa anamiliki watu kutoka eneo hilo ilhali amekuwa akishinda akiwatusi viongozi waliochaguliwa kila mara anapozuru kaunti za maeneo hayo,” akasema.

Bi Shebesh ambaye alikuwa mbunge mwakilishi wa kike wa Nairobi, alisema kauli mbiu ya Azimio la Umoja ambayo inavumishwa na Bw Odinga inalenga kuendeleza maono ya Rais Kenyatta. Kupitia kwa azimio hilo, Wakenya hawatashuhudia machafuko tena jinsi ambavyo ilikuwa katika uchaguzi mkuu wa 2007.

You can share this post!

Madai ya uzinzi yatishia kuvunja ndoa ya Kaparo

Makali ya janga la ukame yawasukuma baadhi ya wanaume...

T L