Habari za Kaunti

Mama kanisa watano wafariki ajalini wakitoka eneo spesheli la Marian

February 4th, 2024 1 min read

NA MWANGI MUIRURI

WINGU la simanzi limetanda katika Kanisa Katoliki tawi la Kaunti ya Murang’a baada ya mama kanisa watano kuaga dunia wakitoka katika hafla ya maombi usiku kucha katika eneo spesheli la kitamaduni la Marian.

Watano hao walikuwa wamekodisha gari la kampuni ya MTN mjini Murang’a kuwasafirisha hadi Kaunti ya Nyandarua kuliko eneo hilo la maombi spesheli ambalo huwavutia waumini wengi.

Katika ripoti ambayo mkuu wa Kanisa hilo Murang’a Askofu Maria Wainaina alitoa, waumini hao waliokuwa 14 katika gari hilo, walikumbana na ajali hiyo mnamo Februari 3, 2024, katika barabara ya kutoka Nyahururu kuenda Nyeri mwendo wa saa mbili usiku.

“Ni kina mama wa Muungano wa Matendo wa Kikatoliki (CWA) wa Kanisa la Gaitega lililoko wadi ya Mbiri. Gari lao lilipoteza mwelekeo na kuanguka na kusababisha mauti hayo huku wengine wakipata majeraha,” akasema Askofu Wainaina.

Aliwaombea wendazao amani ya kudumu huku manusura akiwatakia neema ya uponyaji.

Viongozi wa Kaunti ya Murang’a wakiongozwa na Seneta Joe Nyutu, Mbunge Mwakilishi wa Kike wa Kaunti ya Murang’a Betty Maina, mbunge wa Kiharu ambako kanisa hilo la Gaitega liko Bw Ndindi Nyoro, Waziri wa Ardhi na Nyumba Alice Wahome, Mkurugenzi wa Kampuni ya huduma za maji na usafi la Murang’a Kusini (Muswasco) Mary Nyaga na mbunge wa Maragua Bi Mary wa Maua walitoa risala zao za rambirambi.

Wote waliahidi kushirikiana na walioathirika na ajali hiyo kuafikia heshima za mwisho kwa wendazao na pia katika matibabu ya majeruhi.