Dondoo

Mama, mkaza mwana wapiga dume

November 18th, 2019 1 min read

Na TOBBIE WEKESA

MBUSYANI, KITUI

WENYEJI wa eneo hili walipigwa na butwaa mama mkwe aliposhirikiana na binti yake kumuadhibu polo.

Inasemekana tukio hili lilitokea baada ya polo kumfuata mkewe hadi kwao na kumlazimisha arudi naye.

Kulingana na polo, mke alikuwa ameenda kwao kuwaona wazazi bila ruhusa yake.

Duru zinasema jamaa alipofika kwa wakwe zake alimkuta mkewe ameketi na mamake. Polo alipewa kiti lakini alikataa kuketi.

“Nani alikupatia ruhusa ya kuja kwenu,” polo alimfokea mkewe. Mama mkwe alishindwa kuelewa kilichokuwa kikiendelea.

Polo aliendelea kumfokea mkewe bila kuogopa kwamba mama mkwe yuko hapo. “Lazima ujue kwamba mimi ni mumeo. Kila kitu unachofanya lazima unifahamishe. Nani alikupatia ruhusa ya kuja hapa kwenu?” polo alimuuliza kipusa kwa hasira.

Duru zinasema matamshi ya polo hayakumfurahisha kabisa mkewe. “ Si lazima nikuombe ruhusa kwenda kwetu. Sijui aliyekuroga ni nani. Peleka ujinga na ulevi wako mbali,” kipusa alimzomea kalameni.

Mama mkwe alipoona jamaa amekosa adabu, alimuagiza aondoke mara moja. “Kama huna jambo la maana lililokuleta hapa ondoka upesi,” mama ya mke alimaka.

Habari zilizotufikia zinasema polo alimkaribia mkewe na kumzaba kofi. Kipusa naye alimrukia mumewe na kumuangushia kofi kali. “Mimi si mtoto wako wala mali yako. Huwezi kuja kunipigia kwetu,” mke aliapa.

Mama mkwe alipoona jamaa amezidi aliamua kujiunga na binti yake kumuadhibu. “Huwa nasikia tu kwamba wewe ni mvutaji wa bangi. Leo nimethibitisha hilo. Acha nikuambie, leo utatujua vizuri,” mama huyo alimngurumia jamaa huku akimuangushia viboko mgongoni.

Inadaiwa kalameni alijaribu kujinasua lakini hakutoboa. “Hakuna unachonidai. Shetani wewe,” mama mkwe aliendelea kufoka huku yeye na binti yake wakimtandika jamaa.

Ilibidi majirani waingilie kati ili kumuokoa kalameni.