Habari

Mama, mtoto wafungiwa na ajenti kwa kushindwa kulipa kodi

July 14th, 2020 1 min read

Na PHYLLIS MUSASIA

WAKAZI wa Egerton, Njoro katika Kaunti ya Nakuru wamewashutumu polisi kwa kumwachilia huru ajenti wa nyumba aliyemfungia mwanamke na mwanawe ndani ya nyumba kwa kuchelewa kulipa kodi.

Majirani walisema Benard Omumbo alifika nyumbani kwa Rhoda Makokha mnamo Jumamosi jioni na kuchomelea mlango wa nyumba yake upande wa nje, hivyo kumfungia ndani kutokana na deni la kodi ya Sh10,000.

Mnamo Jumapili mchana, polisi walimwokoa Bi Makokha kutoka ndani ya nyumba hiyo kwa kukata kwa msumeno vyuma vya dirisha.

Baadaye Bi Makokha alipelekwa katika kituo cha polisi cha Njoro alikoandikisha taarifa.

Bw Omumbo alikamatwa na kutarajiwa kufikishwa mahakamani jana, lakini alionekana akitembea mtaani bila wasiwasi wowote.

Bi Makokha aliambia Taifa Leo kuwa baada ya kurejea nyumbani Jumapili, alilazimika kupitia dirishani pamoja na wanawe watano ili kupata pahala pa kulala.

Kulingana naye, siku ya tukio, wanawe wanne walikuwa wanacheza nje nyumba yeye na mtoto mmoja walipofungiwa.

“Huyo ajenti alinikuta ndani ya nyumba siku hiyo nikiwa namuuguza mwanangu wa umri wa miezi 18. Nilimuomba anionee huruma lakini hakutaka kunisikiza. Watoto wanne walilala kwa majirani na rafiki zangu siku hiyo,” akasema.

Majirani walisema si mara ya kwanza kwa ajenti huyo kufanya mambo kama hayo kila mara mpangaji yeyote anapochelewa kulipa kodi.

Bi Makokha alisema deni hilo ni la miezi minne baada ya kukosa ajira tangu Chuo Kikuu cha Egerton kilipofungwa kufuatia janga la ugonjwa wa Covid-19.

“Nilikuwa ninafanya kibarua katika chuo cha Egerton lakini kilipofungwa kazi ikaisha,” akasema.

Kamanda wa polisi wa Njoro, Mohammed Huka alisema ajenti huyo aliachiliwa kwa dhamana ya polisi kwa kuwa wakati huu wa janga la corona hawaruhusu mshukiwa kuzuiliwa seli kwa muda mrefu.

“Mshtakiwa yeyote ana haki ya kuachiliwa kwa dhamana. Polisi wanafanya mpango wa kupata siku ambayo atafikishwa kortini,” akasema Bw Huka.

Hata hivyo hakueleza makosa ambayo ajenti huyo atafunguliwa atakapopelekwa mahakamani.