Habari Mseto

Mama na wanawe wawili wateketea hadi kufa Jomvu

June 23rd, 2020 1 min read

Na MISHI GONGO

MWANAMKE mmoja na wanawe wawili wamefarika baada ya nyumba yao kuteketea katika mtaa wa Jitoni eneo la Jomvu, Kaunti ya Mombasa.

Watatu hao waliokuwa wamepangisha katika jumba la vyumba kumi waliteketea usiku wa Jumatatu.

Akithibitisha tukio hilo, kamanda wa polisi eneo hilo Bw James Mutua amesema walipokea taarifa ya moto huo mwendo wa saa nane usiku kutoka kwa walioshuhudia mkasa huo.

Kamanda huyo amesema walipofika katika eneo la mkasa, alishirikiana na maafisa wa idara ya zimamoto na majirani kujaribu kuuzima moto huo.

“Tulifanikiwa kuzima moto huo lakini tayari watatu hao; mama na watoto wake walikuwa wameshateketea,” amesema.

Alisema mmoja wa watoto alikuwa miaka minne huku wa pili akiwa mwenye umri wa miaka minne.

“Hatujatambua jina la marehemu bado. Maafisa wetu wanaendelea na uchunguzi kujua chanzo cha moto huo,” amesema.