Kimataifa

Mama ndani miaka 9 kwa kunajisi watoto wake kumfurahisha mumewe

February 8th, 2019 1 min read

MASHIRIKA Na PETER MBURU

MWANAMKE kutoka Queensland, Australia ambaye aliwanajisi watoto wake wa kiume na kike alifungwa jela miaka tisa Alhamisi, baada ya kukiri kuwa aliwadhulumu kingono mvulana wake wa miaka 15 na msichana tineja.

Mama huyo wa miaka 51 anasemekana kuwadhulumu watoto hao kwa zaidi ya mwongo ili kumridhisha mumewe aliyekuwa na matatizo ya akili, na kuepuka talaka.

Mwanamume huyo, hata hivyo, alikufa baadaye. Mwanamke huyo Alhamisi alikiri makosa mbele ya korti ambapo alikumbana na mashtaka saba ya unajisi, ambapo alifungwa miaka tisa jela, japo anaweza kuhudumu miaka minne kifungo cha nje.

Msichana ambaye alianza kudhulumiwa kingono akiwa na miaka kumi sasa ana zaidi ya miaka 20. Korti ilielezwa namna alikuwa akijaribu kumbembeleza mamake kuwacha kumdhulumu lakini hakusikia kitu.

Wakati mwingine, mamake angetazama wakati baba alikuwa akimnajisi mtoto huyo, kabla ya kumpa vitambaa ajipanguze.

Tineja huyo aidha alilazimishwa kutazama filamu za ngono na kufanya vitendo vya kingono, korti ikaelezwa. Msichana huyo aliangua vilio mahakamani wakati jaji alikuwa akisoma uamuzi.

Mvulana naye alikuwa akinajisiwa na mamake wiki chache kabla ya babake kufariki.

Daktari wa akili alieleza mahakama kuwa mama huyo hana tatizo lolote la kiakili, lakini akataja uhusiano baina yake na mumewe kama ulemavu wa Stockholm Syndrome, ambapo mdhulumiwa hulazimika kumpenda mtekaji nyara wake.

Jaji David Reid alitaja kesi hiyo kuwa ya kuogofya na mbaya sana ambayo amewahi kushughulikia katika maisha yake.