Mama pabaya kutafuna karo ya wanawe
KAPKOROS, BOMET
POLO wa hapa alimchemkia mkewe kwa kula karo ya shule ya mwanawe, akiamini ufunguzi wa shule ungeahirishwa. Inasemekana mwanadada alimtaka mumewe ampe pesa alizokuwa nazo azichunge ili asifuje.
“Heko! Umetoa jasho mpaka ukapata karo yote ya shule kwa wanetu wote watatu. Lete nikuwekee ili ikifika siku ya kufungua niende kulipa,” alimwambia mumewe.
Polo hakusita, bali alimpa kila kitu na kushusha pumzi kuondokewa na mzigo wa kutafuta karo.
Hata hivyo, siku ya kufungua shule, polo aliduwaa mkewe alipokiri kuwa alitumia pesa hizo.
Mumewe alimsuta sana na kumpa siku chache apate pesa hizo.