Mama Sarah Obama alikuwa mwanamke wa kipekee – Raila Odinga

Na SAMMY WAWERU

TAIFA limepoteza mama na kiongozi aliyestahimili mawimbi ya changamoto kuona familia yake na jamii imeimarika, amesema kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga akimuomboleza Mama Sarah Obama, nyanya ya aliyekuwa Rais wa Amerika, Bw Barack Obama.

Mama Sarah alifariki mapema Jumatatu, katika Hospitali ya Rufaa na Mafunzo ya Jaramogi, Kisumu ambapo alikuwa anapokea matibabu baada ya kuugua kwa muda mfupi.

Aidha, Taifa Leo Dijitali imebaini kuwa alilazwa humo Jumapili asubuhi. Akimuomboleza Mama Sarah, Bw Odinga amemtaja kama mama kiongozi “aliyeishi mbele ya nyakati zake”.

“Alisimama kidete na familia yake baada ya mume wake kuaga dunia. Alionyesha ukakamavu wa mwanamke wa aina yake wa Kiafrika, aliyestahimili mawimbi ya changamoto za maisha,” Bw Odinga akaelezea kupitia taarifa yake ya salamu za pole.

Mama Sarah na ambaye alikuwa mjane, alikuwa mke wa tatu wa babu ya Rais Barrack Obama, Barack Hussein Obama Senior.

“Alitumia fursa ya mjukuu wake kuwa madarakani, Rais Barack Obama kupiga jeki elimu ya mtoto wa kike katika jamii na pia kutoa misaada kwa wasiojiweza, kupitia wakfu wake. Mama Ida (mke wa Bw Odinga) na mimi tunatuma risala za pole kwa familia ya Obama,” akasema kiongozi huyo wa ODM.

Mama Sarah atakumbukwa kutokana na mchango wake mkuu kupitia Wakfu wa Mama Sarah Obama, aliotumia kulipia mayatima karo na watoto wanaotoka familia zisizoweza.

Marehemu pia, akiwa uhai alikuwa akisaidia wajane na familia zisizojiweza, kwa kuwapa vyakula, mavazi na kuwakithi mahitaji mengine muhimu ya kimsingi.

Amefariki akiwa na umri wa miaka 99. Kutokana na mchango wake katika jamii, amepokea tuzo chungu nzima, ngazi ya kitaifa na kimataifa.