Mama Sarah Obama azikwa katika hafla iliyohudhuriwa na wachache

Mama Sarah Obama azikwa katika hafla iliyohudhuriwa na wachache

Na SAMMY WAWERU

NYANYA ya aliyekuwa Rais wa Amerika Bw Barack Obama, Mama Sarah Obama alizikwa Jumanne nyumbani kwake katika kijiji cha Nyang’oma, Kogelo, Kaunti ya Siaya.

Mama Sarah na ambaye alifariki Jumatatu alfajiri, alipumzishwa katika hafla iliyohudhuriwa na watu wachache, wakiwemo watu wa karibu wa familia, jamaa, marafiki, wageni mashuhuri, wanasiasa na baadhi ya viongozi wakuu serikalini.

Kabla hafla ya maziko kuanza, hali ya mshikemshike ilishuhudiwa asubuhi polisi walipozuia baadhi ya wanafamilia kuingia katika boma la mwendazake wakishikilia kwamba yalipaswa kuhudhuriwa na idadi ya watu wasiozidi 30.

Maafisa wa usalama waliweka vizuizi vya barabara zinazoelekea kwake, ili kuzuia raia kuingia, katika kile walisema ni kuzingatia sheria na mikakati iliyowekwa kusaidia kudhibiti maenezi ya virusi vya corona.

“Tumeweka vizuizi katika barabara zinazoelekea kwa Mama Sarah. Wanasiasa hawataruhusiwa kuandamana na wafuasi wao,” akaonya Kamishna wa Kaunti ya Saiya, Bw Michael Ole Tialal.

Wanafamilia waliokuwa wamezuiwa hata hivyo waliruhusiwa kuingia baada ya mazungumzo na kuafikiana.

Mwenyekiti wa Muungano wa Waislamu Kisumu, Sheikh Musa Ismail ndiye aliongoza kumzika Mama Sarah Obama.

Alizikwa kabla ya sita mchana, na kwa mujibu wa mila na itikadi za dini la Kiislamu. Aidha, alizikwa karibu na kaburi la mume wake, marehemu Hussein Onyango Obama.

Waziri wa Ulinzi Bi Raychelle Omamo alikuwa kati ya viongozi wakuu serikalini waliohudhuria hafla hiyo ya kumpa heshima za mwisho Mama Sarah.

Alitoa mchango wa Sh1 milioni kutoka kwa Rais Uhuru Kenyatta, ili kuisaidia familia ya mwendazake. Mama Sarah atakumbukwa kutokana na utendakazi wake, hususan kuinua mtoto wa kike katika jamii.

Alitumia Wakfu wake wa Mama Sarah Obama kusomesha mayatima na watoto wanaotoka katika familia zisizojiweza.

Isitoshe, alikuwa katika mstari wa mbele kusaidia wajane, familia zisizojiweza kwa kuzipa chakula na kuzikithi mahitaji mengine muhimu ya kimsingi.

Alifariki akiwa na umri wa miaka 99.

You can share this post!

Corona ilivyoyasukuma makanisa kuchangamkia teknolojia

Mbunge azishangaa hospitali za umma kusema hazina mitungi...