Habari Mseto

Mama Sarah Obama kuadhimisha umri wa miaka 97

April 21st, 2019 1 min read

Na BRIAN NGUGI

NYANYAKE Rais wa zamani wa Marekani Barack Obama, Bi Sarah Obama leo ataadhimisha miaka 97 tangu kuzaliwa Jumatatu kwenye sherehe ambayo huenda isivutie wanahabari kama miaka ya nyuma.

Akiwa amejawa na tabasamu nyusoni, Bi Obama alisema kuwa bado ana imani ya kuishi miaka kadhaa licha umri wake kuendelea kusonga.

“Bado najihisi mdogo rohoni. Naweza kusakata ngoma jinsi nilivyokuwa nikifanya nikiwa mdogo,” Mama Sarah akaeleza wanahabari wa Taifa Leo waliomtembelea nyumbani kwake katika kijiji cha Nyang’oma, Kogelo, Kaunti ya Siaya.

Akiwa amevalia mavazi ya Kiafrika maarufu kama Ankara, Mama Sarah alionekana buheri wa afya akizungumza kwa ufasaha huku bintiye wa tano Marsat, akieleza Taifa Leo kwamba bado ajuza huyo hufuatilia masuala yanagonga vichwa vya habari nchini ikiwemo mambo yanayomhusu Rais Obama.

“Ujumbe wake kwa Wakenya ni amani na umoja. Yeye husaidia mayatima, walemavu na wasiojiweza katika jamii. Anawataka vijana kukumbatia masomo na kutia bidii maishani,” akasema Bi Marsat huku akifichua kuwa bibi huyo hupenda kula kitoweo cha samaki na maziwa, vyakula ambavyo vimechangia afya yake kuwa imara.

Bi Sarah ambaye ni mke wa tatu wa babu ya Rais Obama, alianza kufahamika mwaka wa 2004 mjukuu wake aliposhinda kiti cha Useneta cha Illinois kisha kushinda Urais 2008.